Google hulindaje faragha yangu na kuweka maelezo yangu yakiwa salama?
Tunajua usalama na faragha ni muhimu kwako - na ni muhimu kwetu, pia. Tunalipatia suala la kuwa na usalama dhabiti kipaumbele na kukupa imani ya kwamba maelezo yako ni salama na utayapata unapoyahitaji.
Tunaendelea kujitahidi ili kuhakikisha usalama thabiti, kulinda faragha yako, na kufanya Google ikufae zaidi. Tunatumia mamia ya mamilioni ya dola kila mwaka kudumisha usalama, na tumewaajiri wataalamu maarufu katika usalama wa data ili kulinda taarifa zako. Tumebuni pia zana zilizo rahisi kutumia za faragha na usalama kama vile Dashibodi ya Google, uthibitishaji wa hatua mbili na mipangilio ya matangazo yaliyowekewa mapendeleo yanayopatikana katika Kituo Changu cha Matangazo. Kwa hivyo, kuhusu suala la taarifa unazoshiriki na Google, uamuzi huwa ni wako.
Unaweza kupata maelezo zaidi kuhusu ulinzi na usalama mtandaoni, ikiwa ni pamoja na jinsi ya kujilinda mwenyewe na familia yako mtandaoni, katika Kituo cha Usalama cha Google .
Pata maelezo zaidi kuhusu jinsi tunavyoweka maelezo yako ya kibinafsi yakiwa ya faragha na salama — na kukuweka kwenye usukani.
Kwa nini akaunti yangu imehusishwa na nchi?
Akaunti yako huhusishwa na nchi (au eneo) kwenye Sheria na Masharti ili tuweze kubaini mambo mawili:
- Mshirika wa Google anayetoa huduma, anayechakata maelezo yako na anayewajibikia kutii sheria za faragha zinazotumika. Kwa kawaida, Google hutoa huduma zake kwa wateja kupitia mojawapo ya kampuni mbili:
- Google Ireland Limited, iwapo unaishi kwenye nchi washirika katika Makubaliano ya Kiuchumi ya Ulaya (nchi za Umoja wa Ulaya pamoja na Aisilandi, Lishensteni na Norwe) au Uswizi
- Google LLC, inayopatikana Marekani, kwa nchi nyingine zote zilizosalia
- Toleo la sheria na masharti yanayosimamia uhusiano wetu, ambayo yanaweza kutofautiana kulingana na sheria za mahali uliko
Kumbuka kwamba huduma za Google hazibadiliki bila kujali mshirika anayetoa huduma au nchi inayohusishwa na akaunti yako.
Kubaini nchi inayohusishwa na akaunti yako
Unapofungua akaunti mpya, tunahusisha akaunti yako na nchi kulingana na mahali ulipofungulia Akaunti yako ya Google. Kwa akaunti ambazo zimedumu kwa angalau mwaka mmoja, tunatumia nchi ambayo kwa kawaida wewe hutumia kufikia huduma za Google — kwa kawaida huwa ni nchi ambayo umekaa kwa muda mrefu katika mwaka mmoja uliopita.
Hali ya kusafiri mara kwa mara kwa kawaida haiathiri nchi inayohusishwa na akaunti yako. Unapohamia kwenye nchi ya kigeni, inaweza kuchukua takribani mwaka mmoja ili uhusiano wa nchi uliko usasishwe.
Iwapo nchi inayohusishwa na akaunti yako hailingani na nchi unakoishi, hali hii inaweza kutokana na tofauti kati ya nchi unakofanyia kazi na nchi unakoishi, kwa sababu umesakinisha Mtandao Pepe wa Faragha (VPN) ili kuficha anwani yako ya IP, au kwa sababu unaishi karibu na mpaka wa eneo. Wasiliana nasi iwapo unaona kuwa nchi inayohusishwa na akaunti yako si sahihi.
Ninawezaje kuondoa maelezo kunihusu kutoka matokeo ya utafutaji ya Google?
Matokeo ya utafutaji Google ni mfano wa maudhui yanayopatikana na umma kwenye wavuti. Mitambo ya kutafuta haiwezi kuondoa maudhui moja kwa moja kutoka kwa tovuti, kwa hivyo kuondoa matokeo ya utafutaji kutoka Google hakuwezi kuondoa maudhui kwenye tovuti. Ikiwa unataka kuondoa chochote kwenye wavuti, unafaa kuwasiliana na msimamizi wa wavuti wa tovuti ambayo maelezo yamechapishwa na umuulize abadilishe. Maudhui yanapoondolewa na Google imetambua mabadiliko, maelezo hayatapatikana katika matokeo ya utafutaji ya Google. Kama una ombi la dharura la kuondoa maudhui, unaweza pia kutembelea ukurasa wetu wa usaidizi ili upate maelezo zaidi.
Je, hoja zangu za utafutaji hutumwa kwenye tovuti ninapobofya matokeo kwenye huduma ya Tafuta na Google?
Ndiyo, katika hali fulani. Unapobofya matokeo ya utafutaji katika huduma ya Tafuta na Google, huenda pia kivinjari chako kikatuma anwani ya Intaneti, au URL, ya ukurasa wa matokeo ya utafutaji kwenye ukurasa lengwa wa wavuti kama URL Iliyoelekeza. Wakati mwingine URL ya ukurasa wa matokeo ya utafutaji inaweza kuwa na hoja uliyoweka ya utafutaji. Ikiwa unatumia Utafutaji wa SSL (kipengele cha Google cha kutafuta kwa usimbaji fiche), mara nyingi, hoja uliyotafuta haitatumwa kama sehemu ya URL katika URL Iliyoelekeza. Kuna baadhi ya hali zisizofuata mkondo huu, kama vile, ikiwa unatumia vivinjari visivyo maarufu sana. Maelezo zaidi kuhusu Utafutaji wa SSL yanaweza kupatikana hapa. Hoja za utafutaji au maelezo yaliyo katika URL Iliyoelekeza yanaweza kupatikana kupitia Google Analytics au kiolesura cha kusanifu programu (API). Aidha, watangazaji wanaweza kupokea maelezo yanayohusiana na maneno muhimu yaliyowafanya watumiaji wabofye tangazo.