Utangulizi

Lengo la Google ni kupanga maelezo ya dunia na kuyafanya yapatikane kwa watu wote ulimwenguni kwa njia inayowafaa. Maelezo ya mahali ulipo ni muhimu katika jitihada hizo. Kuanzia maelekezo unapoendesha gari, kuhakikisha matokeo yako ya utafutaji yanajumuisha vitu vilivyo karibu nawe, hadi kukuonyesha wakati mkahawa una watu wengi, maelezo ya mahali ulipo yanaweza kufanya hali yako ya utumiaji wa huduma za Google ikufae zaidi.

Maelezo ya mahali ulipo pia husaidia katika utendaji wa msingi wa bidhaa, kama vile kuonyesha tovuti katika lugha sahihi au kusaidia kulinda huduma za Google.

Sera ya Faragha ya Google inafafanua jinsi Google inavyotumia data, ikijumuisha maelezo ya mahali ulipo, unapotumia bidhaa na huduma zake. Ukurasa huu unatoa ufafanuzi wa ziada kuhusu maelezo ya mahali ulipo yanayotumiwa na Google na jinsi unavyoweza kudhibiti kutumika kwa maelezo hayo. Baadhi ya kanuni za data huenda zikatofautiana kwa watumiaji walio chini ya miaka 18. Pata maelezo zaidi kwenye Ilani ya Faragha ya Google kuhusu Akaunti za Google na Wasifu Zinazodhibitiwa kupitia Family Link, kwa Watoto na Mwongozo wa Google kuhusu Faragha kwa Vijana.

Je, Google hutumia vipi maelezo ya mahali?

Google hutumia maelezo ya mahali kwa njia tofauti kulingana na huduma au kipengele husika, mipangilio ya kifaa na akaunti ya mtumiaji. Google inaweza kutumia maelezo ya mahali kwa njia kuu zifuatazo.

Kukupa hali ya utumiaji inayokufaa

Google inaweza kutumia au kuhifadhi maelezo ya mahali ulipo ili kutoa huduma muhimu kwa watumiaji wa bidhaa za Google, kama vile kuonyesha matokeo ya utafutaji yanayofaa na kwa haraka zaidi, kubashiri hali ya trafiki kwa safari za kila siku na kupendekeza maudhui yanayomfaa mtumiaji. Kwa mfano, mtu anapotaka kutazama filamu huenda akapendelea ukumbi wa sinema unaopatikana mahali aliko, na wala si katika jiji lingine. Kwenye Ramani za Google, maelezo ya mahali huwasaidia watumiaji kupata mahali mahususi kwenye ramani na kupata maelekezo ya maeneo ambayo wangependa kutembelea.

Kuwawezesha watumiaji kukumbuka maeneo waliyotembelea

Unaweza kukumbuka ulikokwenda ukiwa na kifaa chako kwa kutumia kipengele cha Rekodi ya Maeneo Uliyotembelea. Ili utumie kipengele cha Rekodi ya Maeneo Uliyotembelea, washa Kumbukumbu ya Maeneo Yangu; hiki ni kipengele cha Akaunti ya Google kinachounda ramani binafsi ya maeneo uliyotembelea na njia ulizopitia. Ukiwasha kipengele cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu, maelezo ya eneo mahususi kilipo kifaa chako huhifadhiwa kwenye ramani binafsi, hata wakati hujafungua programu za Google. Unaweza kuangalia na kufuta maelezo haya kwenye Rekodi ya Maeneo Uliyotembelea.

Kuwawezesha watumiaji kupata mambo haraka na kuona matokeo yanayowafaa

Kwa mfano, Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu ni mipangilio ya akaunti ya Google inayowawezesha watumiaji kuhifadhi data ya shughuli zao na maelezo husika kama vile mahali, ili kupata hali ya utumiaji inayowafaa zaidi wanapotumia huduma za Google wakiwa wameingia katika akaunti. Kwa mfano, huduma ya Tafuta na Google huenda ikakuonyesha matokeo yanayohusiana na eneo kwa jumla ulikofanyia utafutaji hapo awali.

Kukuonyesha matangazo yanayokufaa zaidi

Maelezo ya mahali ulipo yanaweza kusaidia Google kukuonyesha matangazo yanayokufaa zaidi. Unapotafuta kitu kama vile "maduka ya viatu yaliyo karibu nami," maelezo ya mahali yanaweza kutumiwa kukuonyesha matangazo kutoka kwa maduka ya viatu yaliyo karibu nawe. Au, unapotafuta bima ya wanyama vipenzi, huenda watangazaji wakaonyesha manufaa tofauti kutegemea na eneo. Pata maelezo zaidi kuhusu jinsi maelezo ya mahali hutumiwa kuonyesha matangazo.

Kuimarisha usalama wa watumiaji

Google hutumia maelezo ya mahali uliko kutoa baadhi ya huduma za msingi, kama vile kulinda akaunti yako kwa kutambua shughuli zisizo za kawaida, au kitendo cha kuingia katika akaunti kinachofanywa katika jiji tofauti.

Kuonyesha yanayovuma kwenye jumuiya, kutoa makadirio na kwa madhumuni ya utafiti, kwa njia isiyotambulisha mtu

Google pia hutumia maelezo ya mahali yaliyojumlishwa na yanayoficha utambulisho wa data kwa madhumuni ya utafiti na kuonyesha yanayovuma kwenye jumuiya.

Ili uone njia zaidi ambavyo maelezo ya mahali hutumika, tembelea Sera ya Faragha ya Google.

Je, kipengele cha maelezo ya mahali kinatumika vipi kwenye kifaa changu na programu zangu za Android?

Unaweza kupata matokeo ya utafutaji ya mahali ulipo, utabiri wa safari zako na mikahawa iliyo karibu nawe kupitia maelezo ya mahali kilipo kifaa. Mipangilio ya kifaa cha Android kwenye simu yako ya mkononi au kompyuta kibao hukuwezesha kubaini iwapo ungependa kipengele cha huduma za mahali kikadirie mahali kilipo kifaa, na pia ikiwa ungependa kuruhusu programu na huduma mahususi zifikie maelezo ya mahali kilipo kifaa chako na iwapo unahitaji kudhibiti matumizi ya data hiyo.

Jinsi unavyoweza kudhibiti idhini ya programu ya kutumia maelezo ya mahali kilipo kifaa

Teua programu mahususi ambazo ungependa zifikie maelezo ya mahali kilipo kifaa katika mipangilio ya kifaa chako cha Android. Kwenye mipangilio, pana vidhibiti vinavyokuwezesha kubaini iwapo programu inaweza kufikia maelezo ya mahali mahususi au panapokadiriwa. Tumeongeza vidhibiti vinavyokuwezesha kubaini iwapo programu inaweza kufikia maelezo ya mahali kilipo kifaa wakati wowote, programu inapotumika tu, ikiwa programu inahitaji kuomba idhini yako kila wakati, au kamwe isifikie data hiyo. Upatikanaji wa mipangilio na vidhibiti hivi unategemea toleo la Android linalotumika kwenye kifaa chako. Pata maelezo zaidi.

Jinsi kipengele cha maelezo ya mahali kilipo kifaa kinavyofanya kazi

Kulingana na mipangilio ya kifaa chako, vifaa vya Android hukadiria mahali uliko kwa kutumia vipengele tofauti, ikiwemo GPS, vitambuzi (kama vile kipima mchapuko, gurudumu tuzi, kipima sumaku na baromita), mawimbi ya mtandao wa simu na mawimbi ya Wi-Fi. Vipengele hivi vinaweza kutumika kukadiria mahali mahususi zaidi uliko kadri iwezekanavyo, kisha data hii hushirikiwa na programu na huduma ambazo umeruhusu kwenye kifaa. Pata maelezo zaidi kuhusu mipangilio ya mahali ya kifaa chako cha Android.

Mawimbi ya mtandao wa simu na mtandao wa Wi-Fi yanaweza kusaidia Android kukadiria mahali kilipo kifaa, hasa iwapo mawimbi ya GPS hayapatikani au si sahihi, ikiwemo mijini palipo na msongamano mkubwa au ndani ya nyumba. Usahihi wa Kipengele cha Google cha Kutambua Mahali (GLA, pia inajulikana kama Huduma za Mahali za Google) ni huduma ya Google inayotumia mawimbi haya kuboresha makadirio ya mahali kilipo kifaa.

Ili kutambua mahali kwa usahihi zaidi unapoiwasha, GLA hukusanya maelezo ya mahali mara kwa mara kutoka kwenye kifaa chako cha Android—ikiwemo GPS na data kuhusu milango ya mitandao ya Wi-Fi, mitandao ya simu na vitambuzi vya kifaa—kwa kutumia kitambulishi cha muda cha kifaa kisichohusishwa na mtu mahususi. GLA hutumia maelezo haya kuboresha usahihi wa utambuzi wa mahali na kutoa huduma zinazotegemea data ya mahali, ikiwemo kuunda ramani za msaragambo za milango ya mitandao ya Wi-Fi na minara ya mitandao ya simu.

Unaweza kuzima kipengele cha GLA wakati wowote katika mipangilio ya mahali kwenye kifaa chako cha Android. Kipengele cha mahali kitaendelea kufanya kazi hata ukizima GLA kwenye kifaa chako cha Android, na kifaa kitatumia GPS na vitambuzi vya kifaa pekee kukadiria mahali.

Google hujuaje mahali nilipo?

Kulingana na bidhaa unazotumia na mipangilio unayoteua, Google inaweza kutumia maelezo tofauti ya mahali kuwezesha bidhaa na huduma unazotumia zikufae zaidi.

Maelezo haya ya mahali yanaweza kutokana na mawimbi ya wakati halisi, kama vile anwani yako ya IP au kutoka kwenye kifaa chako, na pia shughuli zako zilizohifadhiwa kwenye tovuti na huduma za Google. Google hukusanya maelezo ya mahali kilipo kifaa chako kupitia njia kuu zifuatazo.

Kutokana na Anwani yako ya IP

Anwani ya IP, inayojulikana pia kama anwani ya Itifaki ya Intaneti, ni nambari ya kompyuta au kifaa chako iliyotolewa na Mtoa Huduma zako za Intaneti. Anwani za IP hutumiwa kuunganisha kifaa chako kwenye tovuti na huduma unazotumia.

Sawa na huduma zingine nyingi mtandaoni, Google inaweza kutumia maelezo ya eneo la jumla uliko kutoa huduma fulani za msingi—matokeo yanayokufaa, kama vile mtu anapouliza saa, au kudumisha usalama wa akaunti yako kwa kutambua shughuli zisizo za kawaida, kama vile tukio la akaunti yako kufikiwa na mtu aliye katika jiji lingine.

Kumbuka: Kifaa kinahitaji anwani ya IP ili kuweza kutuma na kupokea trafiki kwenye intaneti. Kimsingi, anwani za IP hulingana na maeneo ya kijiografia. Hii ina maana kwamba programu, huduma, au tovuti zozote unazotumia, ikiwemo google.com, zinaweza kukisia na kutumia maelezo fulani kuhusu eneo la jumla uliko kutokana na anwani yako ya IP.

Kutokana na shughuli zako zilizohifadhiwa

Ikiwa umeingia katika Akaunti yako ya Google na umewasha kipengele cha Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu, data ya shughuli zako kwenye tovuti, programu na huduma za Google huenda ikahifadhiwa kwenye Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu katika akaunti yako. Baadhi ya shughuli zinaweza kujumuisha maelezo kuhusu eneo la jumla ambako ulikuwepo ulipokuwa ukitumia huduma ya Google. Unapotafuta kitu ukiwa kwenye eneo la jumla, utafutaji wako utahusisha eneo la angalau kilomita 3 mraba, au utapanuliwa ili eneo husika liwe na angalau watu 1,000. Hii husaidia kulinda faragha yako.

Wakati mwingine, maelezo ya maeneo ambako ulikuwepo ulipofanya utafutaji hapo awali huenda yakatumika kukadiria eneo sahihi kwa utafutaji wako. Kwa mfano, ukitafuta maduka ya kahawa ukiwa Chelsea, huenda Google ikakuonyesha matokeo ya Chelsea katika utafutaji wako wa baadaye.

Unaweza kuangalia na kudhibiti Historia ya Shughuli zako kwenye Wavuti na Programu katika ukurasa wa Shughuli Zangu.

Iwapo hujaingia katika Akaunti yako ya Google, huenda Google ikahifadhi maelezo fulani ya mahali kutokana na utafutaji wako wa awali kwenye kifaa unachotumia ili kukuonyesha matokeo na mapendekezo yanayokufaa. Ukizima uwekaji mapendeleo ya Utafutaji, Google haitatumia shughuli zako za utafutaji za awali kukadiria mahali ulipo. Pata maelezo zaidi kuhusu jinsi ya kutafuta na kuvinjari kwa faragha.

Kutokana na anwani uliyohifadhi ya nyumbani au kazini

Unaweza kuchagua kuhifadhi maelezo ya maeneo muhimu katika Akaunti yako ya Google, kama vile nyumbani au kazini kwako. Ukiweka anwani zako za nyumbani au kazini, zinaweza kutumiwa kukusaidia kufanya mambo kwa urahisi zaidi, kama vile kupata maelekezo au matokeo ya maeneo yaliyo karibu na nyumbani au kazini na kukuonyesha matangazo yanayokufaa zaidi.

Unaweza kubadilisha au kufuta anwani yako ya nyumbani au kazini wakati wowote kwenye Akaunti yako ya Google.

Kwenye kifaa chako

Jinsi programu za Google hutumia maelezo ya mahali kwenye kifaa chako

Vifaa vina mipangilio au ruhusa unazoweza kutumia kuteua programu ambazo ungependa zifikie maelezo ya mahali mahususi uliko, ikijumuisha programu za Google kama vile Tafuta na Ramani. Maelezo haya ya mahali mahususi ni muhimu katika programu, kama vile Ramani za Google, katika kutoa maelekezo au kukuwezesha kupata matokeo ya utafutaji yanayokufaa mahali ulipo. Kwa mfano, utapata matokeo ya utafutaji yanayokufaa kwa vitu kama vile maeneo yaliyo karibu nawe na maelezo kuhusu hali ya hewa, ukiwasha ruhusa au mipangilio ya utambuzi wa mahali mahususi.

iOS na Android zina kipengele cha ruhusa ya mahali katika programu ambacho unaweza kuwasha au kuzima. Unaweza kuruhusu programu kutumia maelezo ya mahali kilipo kifaa chako kwa ajili ya kutoa vipengele na huduma kulingana na mahali ulipo. Kumbuka, wakati mwingine ni muhimu kwa programu kuhifadhi kwa muda data ya mahali mahususi uliko ili kukuonyesha matokeo yanayokufaa kwa haraka, au kuongeza muda wa matumizi ya betri bila haja ya kusasisha maelezo ya mahali kila wakati.

Baadhi ya programu zinahitaji idhini ya kufikia chinichini maelezo ya mahali kilipo kifaa chako, kama vile Tafuta Kifaa Changu, au ikiwa ungependa kutumia vipengele fulani, kama vile Kushiriki Mahali Ulipo.

Ili upate maelezo zaidi kuhusu jinsi kipengele cha mahali kinavyofanya kazi kwenye kifaa chako cha Android, soma makala haya.

Je, data ya Kumbukumbu ya Maeneo Yangu na Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu huhifadhiwa vipi katika Akaunti yangu ya Google?

Katika miezi ijayo na kuendelea mwaka 2024, mipangilio ya Kumbukumbu ya Maeneo Yangu itabadilika. Watumiaji wa sasa wa kipengele cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu wanaarifiwa mabadiliko haya yanapoathiri akaunti zao na watakapoarifiwa, wataanza kuona jina la kipengele cha Rekodi ya Maeneo Uliyotembelea katika mipangilio yao ya akaunti na programu. Kwa wale ambao tayari wanatumia kipengele cha Rekodi ya Maeneo Uliyotembelea, ikiwa ni pamoja na watumiaji waliokiwasha kipengele hicho moja kwa moja, maelezo yaliyotolewa katika ukurasa huu kuhusu data ya mahali katika kipengele cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu yanatumika kwenye utumiaji wao wa kipengele cha Rekodi ya Maeneo Uliyotembelea. Pata maelezo zaidi.

Kumbukumbu ya Maeneo Yangu na Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu

Kumbukumbu ya Maeneo Yangu na Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu ni vipengele vya Akaunti ya Google vinavyotumia maelezo ya mahali. Huu hapa muhtasari wa kila kipengele. Kumbuka, vipengele au bidhaa zingine pia huenda zikakusanya au kuhifadhi maelezo ya mahali.

Kumbukumbu ya Maeneo Yangu

Ukiwasha kipengele cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu, kitaunda Rekodi ya Maeneo Uliyotembelea, ambayo ni ramani binafsi inayokuwezesha kukumbuka maeneo uliyotembelea, njia ulizopitia na safari zako.

Kipengele cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu kimezimwa kwa chaguomsingi. Ukiwasha kipengele cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu, maelezo ya mahali mahususi kilipo kifaa chako huhifadhiwa mara kwa mara, kwa kila kifaa cha mkononi kinachostahiki ambako umewasha kipengele cha Kuonyesha Mahali Ulipo. Maelezo haya ya mahali kilipo kifaa hutumika kuunda Rekodi ya Maeneo Uliyotembelea, hata wakati hutumii programu za Google.

Ili kufanya hali ya utumiaji wa Google iwafae watumiaji wote, Kumbukumbu ya Maeneo Yangu inaweza kutumika

 • kuoyesha maelezo, kama vile saa maarufu na maarifa kuhusu mazingira, kulingana na data ya mahali inayoficha utambulisho
 • kutambua na kuzuia ulaghai na matumizi mabaya
 • kuboresha na kubuni Huduma za Google, ikiwa ni pamoja na bidhaa za matangazo

Kipengele cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu kinaweza pia kusaidia biashara kukadiria uwezekano wa watu kutembelea maduka yao kutokana na tangazo.

Unaweza kukagua, kubadilisha na kufuta yaliyohifadhiwa kwenye Rekodi yako ya Maeneo Uliyotembelea wakati wowote. Ili uangalie ikiwa umewasha kipengele cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu, nenda kwenye Vidhibiti vya Shughuli. Kwenye ukurasa huo, utaweza kudhibiti mipangilio ya Kumbukumbu ya Maeneo Yangu na vifaa vinavyoshiriki maelezo ya mahali vilipo.

Mara ambazo maelezo ya mahali mahususi uliko hukusanywa kupitia kipengele cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu hutofautiana. Kwa mfano, unapotumia maelekezo kwenye Ramani za Google, huenda maelezo hayo yakakusanywa mara kadhaa kwa dakika. Lakini ikiwa hutumii simu yako, maelezo hayo yanaweza kukusanywa mara moja kila baada ya saa chache.

Muda wa kuhifadhiwa kwa data ya Kumbukumbu ya Maeneo Yangu unategemea mipangilio yako—unaweza kuchagua kufuta data hii kiotomatiki baada ya miezi 3, 18 au 36, au kuhifadhi data hadi utakapoifuta.

Kumbuka

Ukizima kipengele cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu

 • Google itaendelea kuhifadhi data yoyote ya awali ya Kumbukumbu ya Maeneo Yangu ambayo umehifadhi hadi utakapoifuta, au itafutwa baada ya muda ambao umechagua kama sehemu ya mipangilio yako ya kufuta data kiotomatiki.
 • Kuzima kipengele cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu hakuathiri jinsi maelezo ya mahali yanavyohifadhiwa au kutumiwa katika Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu au bidhaa nyingine za Google, k.m., kulingana na anwani yako ya IP. Huenda kukawa na maelezo fulani ya mahali yaliyohifadhiwa kupitia mipangilio mingine.

Ili uangalie ikiwa umewasha kipengele cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu, nenda kwenye Vidhibiti vya Shughuli. Pata maelezo zaidi.

Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu

Data ya Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu hutumika kukupa hali ya utumiaji inayokufaa kwenye Ramani, Tafuta na Google na huduma zingine za Google. Inaweza pia kutumika kukuonyesha matangazo yanayokufaa, kulingana na mipangilio yako ya matangazo. Kipengele cha Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu hufanya kazi kwenye vifaa vyako vyote ambavyo umetumia kuingia katika akaunti yako.

Ukiwasha kipengele cha Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu, Google itahifadhi data ya shughuli zako kwenye huduma za Google katika Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu ya akaunti yako. Hii inajumuisha maelezo husika, kama vile eneo kwa jumla ambako ulitumia huduma ya Google.

Kwa mfano, ukitafuta maelezo kuhusu hali ya hewa kisha upate matokeo ya eneo ambalo maelezo yake yametumwa kutoka kwenye kifaa chako, shughuli hii, pamoja na maelezo ya eneo kwa jumla kilipokuwa kifaa chako ulipotafuta, zitahifadhiwa kwenye Historia ya Shughuli zako kwenye Wavuti na Programu. Maelezo ya mahali mahususi yaliyotumwa na kifaa chako hayatahifadhiwa, maelezo ya eneo kwa jumla ndiyo pekee yatakayohifadhiwa. Maelezo ya mahali yaliyohifadhiwa, ambayo huenda yakatumika kuwezesha Google kutambua mahali mahususi zaidi katika utafutaji wa baadaye, yanaweza kutokana na anwani ya IP au kifaa chako. Maelezo ya mahali yaliyohifadhiwa hufutwa kiotomatiki kwenye Historia ya Shughuli yako ya Wavuti na Programu baada ya siku 30.

Data ya Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu husaidia Google kufahamu maeneo ya jumla yanayokufaa, na kujumuisha matokeo ya maeneo hayo unapotekeleza shughuli kama vile utafutaji.

Unaweza kukagua na kufuta maelezo ya mahali na data nyingine iliyohifadhiwa kwenye Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu, au unaweza kuzima kipengele hiki katika Vidhibiti vya Shughuli. Ukizima kipengele cha Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu, data ya shughuli zako za baadaye haitahifadhiwa.

Kumbuka

Unapozima kipengele cha Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu

 • Huenda bado una shughuli zilizohifadhiwa, ambazo zinaweza kutumika hadi uzifute. Unaweza kufuta shughuli hizi wakati wowote. Maelezo yako ya mahali yaliyohifadhiwa bado yatafutwa kiotomatiki baada ya siku 30.
 • Kuzima kipengele cha Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu hakuathiri jinsi maelezo ya mahali yanavyohifadhiwa au kutumiwa na vipengele vingine, kama vile Kumbukumbu ya Maeneo Yangu. Huenda kukawa na maelezo fulani ya mahali yaliyohifadhiwa kupitia vipengele vingine, ikijumuisha anwani ya IP.

Ili uangalie ikiwa umewasha kipengele cha Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu, nenda kwenye Vidhibiti vya Shughuli. Pata maelezo zaidi

Je, Google hutumia vipi maelezo ya mahali yanayoficha utambulisho au ya siri?

Google hutumia maelezo ya mahali yanayoficha utambulisho na ya siri kusaidia kuboresha faragha ya watumiaji. Kawaida, maelezo yanayoficha utambulisho hayawezi kuhusishwa na mtu yeyote. Maelezo yanayoficha utambulisho huenda yakahusishwa na kitambulishi cha kipekee, kama vile mfululizo wa nambari, badala ya maelezo zaidi yanayomtambulisha mtu binafsi kama vile akaunti, jina au anwani ya barua pepe ya mtu binafsi. Google inaweza kutumia maelezo ya mahali yanayoficha utambulisho na ya siri katika bidhaa na huduma zake kwa madhumuni mbalimbali kama vile kuonyesha matangazo au yanayovuma.

Watumiaji wanaweza kuweka upya baadhi ya vitambulishi vinavyoficha utambulisho wa data vinavyohusiana na maelezo ya mahali. Kwa mfano, watumiaji wanaweza kuweka upya baadhi ya vitambulishi vinavyoficha utambulisho wa data kwa kuweka upya vitambulisho vya matangazo kwenye vifaa vyao vya Android. Pia, Google huweka upya kiotomatiki baadhi ya vitambulishi vinavyoficha utambulisho wa data ili kuimarisha faragha ya watumiaji, ikiwemo kwenye GLA, ambayo ni kipengele cha kifaa ambacho watumiaji wanaweza kutumia kuboresha huduma zinazotegemea mahali na usahihi wa utambuzi kwenye vifaa vyao.

Google inaweza kutumia maelezo ya mahali yanayoficha utambulisho, kwa madhumuni mengine. Kwa mfano, watumiaji wanaweza kugusa maeneo kwenye Ramani za Google, k.m., mkahawa au bustani, na kuona yanayovuma katika eneo hilo. Maelezo ya mahali yanayotumika kuchangia yanayovuma, kama vile saa maarufu, hayawezi kumtambulisha mtu binafsi. Iwapo Google haina maelezo ya kutosha kutoa taarifa sahihi inayoficha utambulisho, maelezo hayo hayataonyeshwa kwenye Google.

Zaidi ya hayo, kwa watumiaji walioondoka kwenye akaunti, Google huwapa njia zingine za kudhibiti maelezo yanayohusiana na vivinjari au vifaa vyao, ikiwemo mipangilio ya kuweka mapendeleo ya Utafutaji, mipangilio ya YouTube na mipangilio ya matangazo. Pata maelezo zaidi

Pata maelezo zaidi kuhusu jinsi Google inavyotumia maelezo ya mahali kwenye Sera ya Faragha ya Google. Pata maelezo zaidi kuhusu jinsi Google inavyohifadhi data iliyokusanywa na jinsi Google huficha utambulisho wa data.

Je, Google huhifadhi maelezo ya mahali kwa muda gani?

Sera ya Faragha ya Google inafafanua desturi zetu za kuhifadhi data ya watumiaji, ikijumuisha maelezo ya mahali yanayokusanywa na Google. Maelezo ya mahali huhifadhiwa kwa muda tofauti, kulingana na aina ya data iliyokusanywa, madhumuni yake na jinsi watumiaji huweka mipangilio yao.

Maelezo fulani ya mahali huhifadhiwa kwenye Akaunti yako ya Google hadi utakapoyafuta

 • Kudhibiti kuhifadhiwa na kufutwa kwa data: Kipengele cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu, na cha Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu vina chaguo za kufuta data kiotomatiki, ambazo hukuwezesha kufuta data kiotomatiki baada ya miezi 3, 18 au 36. Unaweza pia kuangalia data hii kwenye sehemu ya Rekodi ya Maeneo Uliyotembelea na Shughuli Zangu, na unaweza kufuta shughuli mahususi au data nyingi upendavyo. Unaweza kubadilisha mipangilio hii au chaguo lako la kufuta kiotomatiki, wakati wowote.
 • Kuhifadhi maelezo ya mahali: Kulingana na bidhaa au huduma ya Google, maelezo ya mahali yanaweza kuhifadhiwa kwenye Akaunti yako ya Google. Kwa mfano, unaweza kuwekea lebo maeneo katika Picha, au kuongeza anwani ya Nyumbani au Kazini kwenye Ramani. Unaweza kufuta maelezo haya ya mahali.

Unapofuta data, Google hufuata sera ya kuiondoa kabisa kwa njia salama kwenye akaunti yako hivyo data hiyo haiwezi kurejeshwa tena. Kwanza, shughuli unayofuta huondolewa ili isionekane, na haitumiki tena kufanya hali yako ya utumiaji ikufae kwenye Google. Kisha, Google huanza mchakato wa kufuta kabisa data hiyo kwa njia salama na kuiondoa kabisa kwenye mifumo ya Google ya kuhifadhi data. Pata maelezo zaidi kuhusu jinsi Google inavyohifadhi data iliyokusanywa.

Maelezo yanayotumika kwa muda

Kwa maelezo mengine ya mahali, kama ilivyoelezwa kwenye sehemu ya Jinsi Google inavyohifadhi data, kuna wakati mwingine ambapo—badala ya kufuta data mwenyewe—Google huhifadhi data kwa muda uliobanishwa kabla ya kuifuta. Muda ambao Google huchukua kabla ya kufuta data kabisa kwa njia salama unategemea aina ya data, kwa mfano:

 • Google huficha utambulisho wa data ya matangazo katika kumbukumbu za seva kwa kuondoa maelezo ya anwani ya IP baada ya miezi 9 na maelezo ya vidakuzi baada ya miezi 18.
 • Google hufuta maelezo ya mahali yanayotokana na IP na mahali kilipo kifaa kwenye Historia ya Shughuli zako kwenye Wavuti na Programu baada ya siku 30.

Maelezo yanayohifadhiwa kwa kipindi cha muda mrefu kwa madhumuni maalum

Kama ilivyofafanuliwa katika Sera ya Faragha ya Google, “Google huhifadhi data fulani kwa muda mrefu zaidi, ikihitajika, kwa madhumuni halali ya kibiashara au kisheria, kama vile usalama, kuzuia ulaghai na matumizi mabaya, au kuhifadhi rekodi za kifedha." Pata maelezo zaidi kuhusu desturi zetu za kuhifadhi data

Je, maelezo ya mahali hutumika vipi katika matangazo?

Kutuwezesha kukuonyesha matangazo yanayokufaa

Matangazo unayoona yanaweza kutokana na data ya maelezo ya mahali ulipo. Kwa ujumla, maelezo ya mahali yanayotumiwa katika matangazo kwenye Google yanatumika pia kwenye bidhaa ambako matangazo hayo yanaonyeshwa. Kwa mfano, kulingana na mipangilio yako, matangazo unayoonyeshwa kwenye huduma ya Tafuta na mifumo mingine ya Google, yanaweza kutokana na maelezo ya mahali kutoka kwenye kifaa chako, anwani yako ya IP, shughuli zako za awali au maelezo ya anwani yako ya nyumbani na kazini yaliyohifadhiwa katika Akaunti yako ya Google. Zaidi ya hayo, metadata (k.m., saa za eneo zilivyo kwenye kivinjari, kikoa, maudhui ya ukurasa, aina ya kivinjari, lugha ya ukurasa) inaweza kutumika kukadiria nchi uliko au eneo linalokuvutia kwa jumla. Tunaweza kutegemea metadata hii pamoja na ishara za mahali tunazopata kwenye anwani yako ya IP, VPN, huduma mbadala au maelezo mengine ya mtandao.

Kutumia maelezo ya mahali husaidia kukuonyesha matangazo yanayokufaa kulingana na mahali ulipo, au maeneo muhimu kwako. Kwa mfano, ukitafuta mikahawa iliyo karibu nawe kwenye Google kipengele cha mahali kikiwa kimewashwa katika kifaa chako, maelezo ya mahali kilipo kifaa chako yanaweza kutumika kukuonyesha matangazo ya mikahawa iliyo karibu nawe. Maelezo ya mahali ulipo yanaweza pia kutumika kukuonyesha umbali wa biashara zilizo karibu nawe katika matangazo kwenye Google.

Google inaweza pia kutumia historia yako ya kuvinjari au shughuli zako za awali kwenye programu (kama vile mambo uliyotafuta, tovuti ulizotembelea au video ulizotazama kwenye YouTube) na maelezo ya eneo kwa jumla yaliyohifadhiwa katika Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu ili kukuonyesha matangazo yanayokufaa zaidi. Kwa mfano, ukitafuta duka la maziwa lililo karibu nawe kwenye Google, huenda ukaona matangazo ya maduka ya vyakula yanayopatikana katika eneo lako kwa jumla ambako unavinjari Tafuta na Google mara kwa mara ukisubiri basi au treni.

Watangazaji wanaweza tu kulenga matangazo kwenye maeneo ya jumla, kama vile nchi, miji au maeneo yaliyo karibu na biashara zao.

Ili upate maelezo ya ziada kuhusu Mtandao wetu wa Maonyesho, tembelea Kituo cha Usaidizi.

Kuwasaidia watangazaji kupima utendaji

Google inaweza pia kutumia maelezo ya mahali kwa madhumuni ya uchanganuzi na vipimo ili kuelewa jinsi huduma za Google zinavyotumika. ​Kwa mfano, ukiwasha kipengele cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu, Google hutumia data hii kusaidia watangazaji kukadiria uwezekano wa wateja kutembelea maduka yao kutokana na matangazo ya mtandaoni. Makadirio yanayoficha utambulisho wa data ndiyo pekee hushirikiwa na watangazaji, hakuna taarifa binafsi zinazoshirikiwa. Ili kutekeleza hili, Google huhisisha data ya shughuli zako mtandaoni, kama vile kubofya matangazo na data ya Kumbukumbu ya Maeneo Yangu inayohusiana na maduka ya watangazaji. Data ya Kumbukumbu ya Maeneo Yangu haishirikiwi na watangazaji.

Kuboresha bidhaa na huduma za Google

Google pia hutumia maelezo ya mahali kuboresha huduma zake za matangazo. Kwa mfano, data kuhusu matangazo unayotazama, ikijumuisha eneo la jumla la shughuli husika, ambayo huhifadhiwa kwenye akaunti yako inaweza kujumlishwa na kutumika katika mifumo ya mashine kujifunza ambayo huboresha zana za Smart Bidding. Data ya akaunti yako haishirikiwi na watangazaji.

Je, ninaweza kudhibiti vipi jinsi maelezo ya mahali nilipo yanavyotumiwa kunionyesha matangazo?

Unaweza kudhibiti jinsi data ya maeneo yako ya jumla ambako ulitumia tovuti na programu za Google hapo awali inaweza kutumika kukuonyesha matangazo, kwa kukagua kidhibiti cha Maeneo ulikotumia huduma za Google kwenye ukurasa wa Kituo Changu cha Matangazo.

Wakati kipengele cha Maeneo ulikotumia Huduma za Google kimewashwa

Unapowasha kipengele cha Kuweka Mapendeleo ya Matangazo na Maeneo Ulikotumia Huduma za Google, Google itatumia data iliyohifadhiwa katika Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu inayohusiana na maeneo ya jumla ambako ulitumia tovuti na programu za Google kuweka mapendeleo ya matangazo.

Wakati kipengele cha Maeneo ulikotumia Huduma za Google kimezimwa

Ukizima kipengele cha Kuweka Mapendeleo ya Matangazo au Maeneo Ulikotumia Huduma za Google, Google haitatumia data iliyohifadhiwa katika Historia ya Shughuli zako kwenye Wavuti na Programu inayohusiana na maeneo kwa jumla ambako ulitumia tovuti na programu za Google kuweka mapendeleo ya matangazo. Hata ukizima kipengele cha Maeneo Ulikotumia Huduma za Google, huenda bado ukaona matangazo kulingana na maelezo ya mahali ulipo na ya anwani yako ya nyumbani na kazini yaliyohifadhiwa katika Akaunti yako ya Google.

Pia, iwapo umeondoka kwenye akaunti, huenda Google bado ikatumia maelezo ya mahali ulipo kupitia anwani yako ya IP au kifaa chako kukuonyesha matangazo kulingana na mipangilio ya kifaa chako na programu yako.

Ili upate maelezo zaidi kuhusu jinsi ya kuwasha na kuzima uwekaji mapendeleo ya matangazo ukiwa umeondoka kwenye akaunti, soma makala haya.

Programu za Google
Menyu kuu