Jinsi Google inavyotumia taarifa ya mahali
- Kwa nini Google hutumia taarifa za mahali?
- Google hujuaje mahali nilipo?
- Je, mahali huhifadhiwa vipi katika Akaunti yangu ya Google?
- Je, mahali hutumika vipi ili kuonyesha matangazo?
Kwa nini Google hutumia taarifa za mahali?
Sera ya Faragha ya Google huelezea namna tunavyoshughulika na taarifa unapotumia bidhaa na huduma za Google, ikiwa ni pamoja na taarifa za mahali. Ukurasa huu hutoa taarifa za ziada kuhusu taarifa za mahali tunazokusanya na namna unavyoweza kuzidhibiti.
Kutoa hali muhimu na zinazofaa za utumiaji ni jambo la msingi ambalo Google hufanya na taarifa za mahali zina jukumu muhimu kutekeleza hilo. Kuanzia maelekezo ya kuendesha gari, kuhakikisha kuwa matokeo yako ya utafutaji yanajumuisha vitu vilivyo karibu nawe, kukuonyesha wakati ambapo mkahawa una shughuli nyingi, taarifa za mahali zinaweza kufanya hali zako za utumiaji kote kwenye Google kukufaa na muhimu zaidi. Taarifa za mahali pia husaidia kwa utendajikazi wa msingi wa bidhaa, kama vile kutoa tovuti katika lugha sahihi au kusaidia kulinda huduma za Google.
Google hujuaje mahali nilipo?
Kutegemea bidhaa unayotumia na mipangilio unayochagua, unaweza kuipa Google aina tofauti za taarifa za mahali ambazo ni muhimu sana ili kufanya baadhi ya huduma kufanya kazi na nyingine kukufaa zaidi. Taarifa za mahali zinaweza kutokana na ishara za muda halisi, kama vile Anwani ya IP au mahali kifaa kilipo na pia shughuli zako za awali kwenye tovuti na huduma za Google ili kufaa muktadha wako. Zifuatazo ni njia za msingi ambazo tunaweza kutumia kupata taarifa kuhusu mahali ulipo.
Kutoka kwenye Anwani ya IP ya Muunganisho wako wa Intaneti
Anwani ya IP (ambayo pia inaitwa anwani ya Intaneti) hukabidhiwa kifaa chako na Mtoa Huduma za Intaneti na inahitajika ili uweze kutumia intaneti. Anwani za IP hutumiwa kuweka muunganisho kati ya kifaa chako na tovuti na huduma unazotumia. Anwani za IP hutokana kimsingi na maeneo ya kijiografia. Hii inamaanisha kuwa tovuti yoyote unayotumia, ikiwemo google.com, inaweza kupata taarifa kuhusu eneo la jumla ambako uko.
Jinsi zilivyo huduma nyingine nyingi za intaneti, Google inaweza kutumia taarifa kuhusu eneo la jumla ambako uko ili kutoa baadhi ya huduma za msingi. Kukadiria eneo la jumla ambako uko kunamaanisha kuwa Google inaweza kukupa matokeo yanayofaa na kuimarisha usalama wa akaunti yako kwa kutambua shughuli zisizo za kawaida, kama vile tukio la kuingia katika akaunti kwenye jiji tofauti.
Kutokana na shughuli zako za awali
Unavyoendelea kutumia huduma zetu, tunaweza kukisia kuwa unavutiwa na eneo fulani hata kama kifaa chako hakituelezi mahali mahususi ulipo. Kwa mfano, ukitafuta "Migahawa Jijini Paris", tunaweza kukisia kuwa ungependa kuona maeneo yaliyo karibu na Paris na kukuonyesha matokeo ya migahawa iliyo huko. Baadhi ya vipengee vinavyotokana na shughuli zako, kama vile utafutaji wa awali, vinaweza pia kuwa eneo la jumla ambako ulikuwa wakati huo. Kulingana na mipangilio yako, aina hii ya taarifa inaweza kuhifadhiwa kwenye akaunti yako na itumiwe kama data, kama vile kuamua iwapo bado uko Paris unapofanya utafutaji zaidi baadaye.
Kutoka kwenye maeneo uliyowekewa lebo
Pia unaweza kuchagua kutuambia kuhusu maeneo ambayo ni muhimu kwako, kama vile nyumbani au kazini kwako. Hii inaweza kukusaidia kufanya mambo kama vile kuonyesha maelekezo ya maeneo haraka kwa kuonyesha kiotomatiki anwani za nyumbani na kazini kwako. Taarifa hii inaweza kutumika pia kuathiri matokeo tunayokupa. Pata maelezo zaidi
Kutoka kwenye vifaa vyako
Vifaa vingi, kama vile simu au kompyuta, vinaweza kubaini eneo mahususi vilipo. Unaweza kuruhusu Google na programu nyingine zikupe vipengele muhimu kulingana na mahali ambapo kifaa chako kipo. Kwa mfano, ikiwa unachelewa kukutana na marafiki zako, pengine utahitaji kutumia programu ya maelekezo ili kujua njia ya haraka zaidi ya kufika unakoenda. Ili kupata maelekezo ya hatua kwa hatua, unaweza kuhitajika kuwasha kipengele cha mahali katika kifaa chako na kuipa programu ruhusa ya kufikia. Au, kwa baadhi ya utafutaji kama vile “duka la kahawa”, “kituo cha mabasi” au “ATM”, matokeo yatakuwa ya maana zaidi wakati eneo mahususi litapatikana.
Kwenye kifaa chako cha Android, ukichagua kuwasha mahali kifaa chako kilipo, unaweza kutumia vipengele kama vile maelekezo, kuipa programu uwezo wa kufikia mahali ulipo sasa, au kuipata simu yako. Pia, unaweza kuchagua programu zilizo na ruhusa ya kutumia mahali kifaa chako kilipo kwa kutumia vidhibiti nyepesi ambavyo vinakuwezesha kuzima au kuwasha ruhusa kwa programu mahususi. Kwenye Android, unaweza kuona wakati ambapo programu inaomba kutumia mahali simu yako ilipo kulingana na GPS wakati sehemu ya juu ya skrini yako inaonyesha Mahali. Pata maelezo zaidi
Huduma za Mahali za Google
Kwenye vifaa vingi vya Android, Google, kama mtoa huduma wa mtandao wa mahali, hutoa huduma ya mahali inayoitwa Huduma za Mahali za Google (GLS). Katika matoleo ya Android 9 na mapya zaidi, huduma hii hujulikana kama Usahihi wa Kipengele cha Google cha Kutambua Mahali. Huduma hii hulenga kuonyesha mahali sahihi zaidi kifaa kilipo na kuboresha usahihi wa mahali kwa ujumla. Simu nyingi za mkononi huwa na GPS, ambayo hutumia ishara kutoka kwenye setilaiti ili kutambua mahali kifaa kilipo – hata hivyo, kwa kutumia Huduma za Mahali za Google, taarifa za ziada kutoka kwenye Wi-Fi, mitandao ya simu na vitambuzi vya vifaa vilivyo karibu zinaweza kukusanywa ili kutambua mahali kifaa chako kilipo. Hufanya hivi mara kwa mara inapokusanya data ya mahali kutoka kwenye kifaa chako na kuitumia kwa njia isiyokutambulisha ili kuboresha usahihi wa mahali.
Unaweza kuzima Huduma za Mahali za Google wakati wowote katika mipangilio ya mahali ya kifaa chako. Mahali kifaa chako kilipo pataendelea kufanya kazi hata kama GLS imezimwa, lakini kifaa kitategemea GPS pekee ili kukadiria mahali kifaa kilipo kwa programu zilizo na ruhusa inayohitajika. Huduma za Mahali za Google ni tofauti na mipangilio ya mahali ya kifaa chako. Pata maelezo zaidi
Mipangilio na ruhusa katika kidhibiti cha Android iwe vitambuzi vya kifaa chako (kama vile GPS) au mahali penye mtandao (kama vile GLS) vimetumika kutambua mahali ulipo na programu zilizo na ruhusa ya kufikia mahali hapo. Haiathiri jinsi tovuti na programu zinaweza kukadiria eneo uliko kwa njia nyingine, kama vile kutoka kwenye Anwani yako ya IP.
Je, mahali huhifadhiwa vipi katika Akaunti yangu ya Google?
Kutegemea bidhaa na huduma za Google ambazo unatumia na mipangilio yako, Google inaweza kuhifadhi taarifa za mahali kwenye Akaunti yako ya Google. Maeneo mawili kati ya maeneo yanayofahamika sana ambapo taarifa hii inaweza kuhifadhiwa ni Kumbukumbu ya Maeneo Yangu na Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu.
Kumbukumbu ya Maeneo Yangu kwenye Google
Ikiwa utachagua kuingia katika Kumbukumbu ya Maeneo Yangu na kifaa chako kinaripoti mahali, taarifa sahihi za mahali pa vifaa vyako vilivyoingia kwenye akaunti zitakusanywa na kuhifadhiwa, hata wakati ambapo hutumii bidhaa au huduma ya Google kwa ukamilifu. Hatua hiyo husaidia kuunda Rekodi yako ya Maeneo Uliyotembelea mahali ambapo data ya Kumbukumbu ya Maeneo Yangu huhifadhiwa na huweza kutumiwa kuyapa nguvu mapendekezo ya wakati ujao kwenye Google. Unaweza kukagua, kubadilisha na kufuta kile ambacho kimehifadhiwa kwenye Rekodi yako ya Maeneo Uliyotembelea wakati wowote.
Kuwasha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu hukupa hali za utumiaji zilizoboreshwa kwenye huduma zote za Google kama vile mikahawa inayopendekezwa kwenye Ramani za Google kulingana na maeneo uliyokwenda kutembelea, taarifa za wakati halisi kuhusu wakati mzuri wa kwenda nyumbani au kazini ili kuepuka msongamano wa magari barabarani na albamu katika Picha kwenye Google ambazo zimeundwa kiotomatiki kutoka katika sehemu ulizotembelea.
Ili kutambua ikiwa umewasha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu, tembelea Vidhibiti vyako vya shughuli. Unaweza kuombwa kuingia kwenye akaunti na baada ya hapo, unaweza kuona iwapo kidhibiti hiki kimewashwa. Ingawa unaweza kusitisha mkusanyiko wa data mpya ya Kumbukumbu ya Maeneo Yangu, data ya zamani ya Kumbukumbu ya Maeneo Yangu itaendelea kuhifadhiwa hadi utakapoifuta. Pata maelezo zaidi
Ukifuta data ya Kumbukumbu ya Maeneo Yangu, bado unaweza kuhifadhi data nyingine ya mahali kwingine kama vile katika Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu.
Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu
Ikiwa Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu imewashwa, matokeo yako ya utafutaji na shughuli kutoka katika huduma nyingine za Google huhifadhiwa kwenye Akaunti yako ya Google. Shughuli iliyohifadhiwa katika Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu pia huweza kujumuisha taarifa ya mahali. Kama mfano, ukiandika 'hali ya hewa' kwenye Tafuta na Google na kupata matokeo ya utafutaji kulingana na mahali ulipo, shughuli hii, ikiwa ni pamoja na mahali palipotumika kutoa matokeo haya, huhifadhiwa kwenye Historia yako ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu. Mahali palipotumika na kuhifadhiwa pamoja na Historia yako ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu panaweza kuonekana kutoka kwenye ishara kama vile anwani ya IP ya kifaa, shughuli yako ya awali, au kutoka kwenye kifaa chako, ikiwa umechagua kuwasha mipangilio ya mahali kifaa chako kilipo.
Kuwasha mipangilio ya Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu hutusaidia kukuonyesha matokeo muhimu ya utafutaji, matangazo yanayokufaa zaidi na mapendekezo yanayokutumikia utakavyo zaidi kama vile unapoona utafutaji wako umependekezwa kiotomatiki kulingana na mambo uliyotafuta awali. Unaweza kukagua na kufuta kile ambacho kipo kwenye Historia yako ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu au kuisitisha kwenye Akaunti yako ya Google. Kusimamisha kwa muda Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu kutasitisha kuhifadhi utafutaji wako wa siku zijazo na shughuli kutoka katika huduma nyingine za Google. Hata kama utafuta data yako ya Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu, bado unaweza kuhifadhi data ya mahali kwingine kama vile kwenye Kumbukumbu ya Maeneo Yangu.
Ili kuelewa ikiwa umewasha Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu, tembelea Vidhibiti vyako vya shughuli. Unaweza kuombwa kuingia kwenye akaunti na baada ya hapo, unaweza kuona iwapo kidhibiti hiki kimewashwa. Pata maelezo zaidi
Je, mahali hutumika vipi ili kuonyesha matangazo?
Matangazo yanaweza kutolewa kulingana na mahali ulipo kwa jumla. Inaweza kujumuisha mahali palipoonyeshwa kutoka kwenye anwani ya IP ya kifaa. Kutegemea mipangilio yako ya kuweka mapendeleo ya matangazo, pia unaweza kuona matangazo kulingana na shughuli kwenye Akaunti yako ya Google. Inajumuisha shughuli iliyohifadhiwa katika Historia yako ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu, ambayo inaweza kutumika kwa ajili ya matangazo muhimu zaidi. Mfano mwingine ni ikiwa umewasha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu na kuvinjari mara kwa mara maeneo ya mchezo wa kuteleza kwenye theluji, huenda baadaye ukaona tangazo kuhusu vifaa vya mchezo huu unapotazama video kwenye YouTube. Google pia hutumia Kumbukumbu ya Maeneo Yangu kwa namna ya kujumlisha na isiyoweza kutambulisha kwa watumiaji walioichagua ili kuwezesha watangazaji kupima mara ambazo kampeni ya matangazo kwenye mtandao inavyosaidia kuelekeza shughuli kwenye biashara au maduka yao halisi. Hatushiriki na watangazaji kipengele chako cha Kumbukumbu ya Maeneo Yangu wala taarifa nyingine zinazoweza kukutambulisha.
Unadhibiti data iliyohifadhiwa kwenye Akaunti yako ya Google na unaweza kuzima matangazo yanayokufaa wakati wowote. Wakati kipengele cha kuweka mapendeleo ya matangazo kimezimwa, Google haitumii data iliyohifadhiwa kwenye Akaunti yako ya Google ili kukupa matangazo yanayokufaa zaidi.