Jinsi Google inavyoshughulikia maombi ya serikali kuhusu maelezo ya watumiaji

Mashirika ya serikali kote duniani huiomba Google ifichue maelezo ya watumiaji. Tunakagua kwa umakini kila ombi ili kuhakikisha kuwa linatii sheria zote zinazotumika. Iwapo ombi linataka maelezo mengi mno, tunajaribu kuyapunguza na katika hali zingine, tunakataa kutoa maelezo yoyote kabisa. Tunashiriki idadi na aina ya maombi tunayopokea kwenye Ripoti yetu ya Uwazi.

Jinsi tunavyoshughulikia ombi hutegemea anayekupa huduma za Google — kwa bidhaa zetu nyingi, huduma hutolewa na Google LLC, kampuni iliyo Marekani inayohudumu chini ya sheria ya Marekani au Google Ireland Limited, kampuni iliyo Ayalandi inayohudumu chini ya sheria ya Ayalandi. Ili utambue mtoa huduma wako, soma Sheria na Masharti ya Google au uwasiliane na msimamizi wa akaunti iwapo Akaunti yako ya Google inasimamiwa na shirika.

Tunapopokea ombi kutoka kwa shirika la serikali, tunatuma barua pepe kwa akaunti ya mtumiaji kabla ya kufichua maelezo. Iwapo akaunti inasimamiwa na shirika, tutatuma ilani kwa msimamizi wa akaunti.

Hatutatuma ilani iwapo tumekatazwa kisheria chini ya sheria na masharti ya ombi. Tutatuma ilani baada ya kuondolewa kwa marufuku ya kisheria, kama vile kuisha kwa kipindi cha sheria au kizuizi kilichoamriwa na mahakama.

Huenda tukakosa kutoa ilani iwapo akaunti imezimwa au kudukuliwa. Na huenda tukakosa kutoa ilani katika hali za dharura, kama vile matishio kwa usalama wa mtoto au matishio kwa maisha ya mtu na tutatoa ilani baada ya kufahamu kuwa kipindi cha dharura kimepita.

Maombi yanayotumwa na mashirika ya serikali ya Marekani katika kesi za madai, usimamizi na jinai

Marekebisho ya Nne ya Katiba ya Marekani na Sheria ya Faragha ya Mawasiliano ya Kielektroniki (ECPA) hudhibiti uwezo wa serikali wa kumlazimisha mtoa huduma kufichua maelezo ya watumiaji. Mamlaka za Marekani zinapaswa kufanya angalau mambo yafuatayo:

  • Katika kesi zote: Kutoa amri ya kufika mahakamani ili kulazimisha ufumbuzi wa maelezo ya msingi ya usajili wa mtumiaji na anwani fulani za IP
  • Katika kesi za uhalifu
    • Kupata amri ya mahakama ya kulazimisha ufumbuzi wa rekodi zisizo za maudhui, kama vile sehemu za barua pepe za Kwa, Kutoka Kwa, Nakala Kwa, Nakala Fiche Kwa na Muhuri wa muda
    • Kupata idhini ya kusaka ya kulazimisha ufumbuzi wa maudhui ya mawasiliano, kama vile picha, hati na ujumbe wa barua pepe

Maombi yanayotumwa na mashirika ya serikali ya Marekani katika kesi zinazohusisha usalama wa taifa

Katika uchunguzi unaohusiana na usalama wa taifa, serikali ya Marekani inaweza kutumia Barua ya Usalama wa Taifa (NSL) au mojawapo ya mamlaka zilizotolewa chini ya Sheria ya Uchunguzi wa Upelelezi wa Nchi za Kigeni (FISA) ili kuilazimisha Google itoe maelezo ya watumiaji.

  • NSL haihitaji idhini ya mahakama na inaweza tu kutumiwa kutulazimisha tutoe maelezo machache ya mtumiaji.
  • Idhini na amri za FISA zinaweza kutumika kulazimisha uchunguzi wa kielektroniki na ufumbuzi wa data iliyohifadhiwa, ikiwa ni pamoja na maudhui kutoka kwenye huduma kama vile Gmail, Hifadhi na programu ya Picha kwenye Google.

Maombi yanayotumwa na mamlaka za serikali nje ya Marekani

Wakati mwingine, Google LLC hupokea maombi ya ufumbuzi wa data kutoka kwa mamlaka za serikali nje ya Marekani. Tunapopokea mojawapo ya maombi haya, tunaweza kutoa maelezo ya mtumiaji iwapo hatua hii inalingana na mambo yote yafuatayo:

  • Sheria ya Marekani, inayomaanisha kuwa ufikiaji na ufumbuzi unaruhusiwa chini ya sheria za Marekani zinazotumika, kama vile Sheria ya Faragha ya Mawasiliano ya Kielektroniki (ECPA)
  • Sheria ya nchi ambako ombi linatoka inayomaanisha kuwa tunahitaji mamlaka ifuate mchakato sawa na mahitaji ya kisheria ambayo yangetumika iwapo ombi lingetumwa kwa mtoa huduma wa nchini anayetoa huduma sawa
  • Kanuni za kimataifa zinazomaanisha kuwa tunatoa tu data kulingana na maombi yanayotimiza Kanuni za Uhuru wa Kujieleza na Faragha za Mpango wa Mtandao wa Dunia na mwongozo wake wa utekelezaji
  • Sera za Google zikiwa ni pamoja na sheria na masharti na sera zote za faragha zinazotumika, pamoja na sera zinazohusiana na ulinzi wa uhuru wa kujieleza

Google Ireland pia hupokea maombi ya maelezo ya watumiaji kwa sababu ina wajibu wa kutoa huduma nyingi za Google kwenye Nchi Washirika katika Makubaliano ya Kiuchumi ya Ulaya na Uswisi.

Maombi yanayotumwa na mashirika ya serikali ya Ayalandi

Google Ireland huzingatia sheria ya Ayalandi inapotathmini maombi ya maelezo ya watumiaji yanayotumwa na shirika la Ayalandi. Sheria ya Ayalandi hutaka mamlaka za utekelezaji wa sheria za Ayalandi zipate amri ya idhini ya mahakama ya kuilazimisha Google Ireland itoe maelezo ya watumiaji.

Maombi yanayotumwa na mamlaka za serikali nje ya Ayalandi

Google Ireland hutoa huduma kwa watumiaji wanaopatikana kote kwenye Nchi Washirika katika Makubaliano ya Kiuchumi ya Ulaya na Uswisi na wakati mwingine tunapokea maombi ya ufumbuzi wa data yanayotumwa na mamlaka za serikali nje ya Ayalandi. Katika hali hii, tunaweza kutoa data ya mtumiaji iwapo hatua hii inalingana na mambo yote yafuatayo:

  • Sheria ya Ayalandi, inayomaanisha kuwa ufikiaji na ufumbuzi unaruhusiwa chini ya sheria za Ayalandi zinazotumika, kama vile Sheria za Jinai za Ayalandi
  • Sheria ya Umoja wa Ulaya (EU) inayotumika Ayalandi, inayomaanisha sheria yoyote ya Umoja wa Ulaya inayotumika Ayalandi ikiwa ni pamoja na Sheria ya Jumla ya Ulinzi wa Data (GDPR)
  • Sheria ya nchi ambako ombi linatoka inayomaanisha kuwa tunahitaji mamlaka ifuate mchakato sawa na mahitaji ya kisheria ambayo yangetumika iwapo ombi lingetumwa kwa mtoa huduma wa nchini anayetoa huduma sawa
  • Kanuni za kimataifa zinazomaanisha kuwa tunatoa tu data kulingana na maombi yanayotimiza Kanuni za Uhuru wa Kujieleza na Faragha za Mpango wa Mtandao wa Dunia na mwongozo wake wa utekelezaji
  • Sera za Google zikiwa ni pamoja na sheria na masharti na sera zote za faragha zinazotumika, pamoja na sera zinazohusiana na ulinzi wa uhuru wa kujieleza

Iwapo tunaamini kwa njia adilifu kuwa tunaweza kuzuia kifo cha mtu au madhara makali ya kimwili, tunaweza kutoa maelezo kwa shirika la serikali — kwa mfano, katika hali za vitisho vya kutokea kwa mlipuko, ufyatuaji wa risasi shuleni, kutekwa nyara, kuzuia kujiua na hali za kutoweka kwa watu. Bado tunashughulikia maombi haya kwa kuzingatia sheria zinazotumika na sera zetu.

Programu za Google
Menyu kuu