Sheria na Masharti ya Google

Inatumika kuanzia 22 Mei 2024 | Matoleo yaliyowekwa kwenye kumbukumbu | Pakua PDF

Toleo la nchi: Marekani

Mambo yanayoshughulikiwa katika sheria na masharti haya

Tunafahamu kuwa unaweza kutaka kuruka Sheria na Masharti haya, lakini ni muhimu ujue mambo unayofaa kutarajia kutoka kwetu unapotumia huduma za Google na mambo tunayotarajia kutoka kwako.

Sheria na Masharti haya yanaonyesha jinsi biashara ya Google hufanya kazi, sheria zinazotumika katika kampuni yetu na mambo fulani ambayo tunaamini kila mara kuwa ya kweli. Kutokana na hayo, Sheria na Masharti haya yanasaidia kufafanua uhusiano wako na Google unapotumia huduma zetu. Kwa mfano, sheria na masharti haya yana mada zifuatazo:

Ni muhimu uelewe masharti haya kwa sababu, kwa kufikia au kutumia huduma zetu (iwe umeingia katika akaunti ya Google au la), unakubali masharti haya.

Mbali na sheria na masharti haya, pia huwa tunachapisha Sera ya Faragha. Tunakuhimiza uisome ili uelewe kwa njia bora jinsi unavyoweza kusasisha, kudhibiti, kuhamisha na kufuta taarifa zako.

Masharti

Mtoa huduma

Huduma za Google zinatolewa na, na unaingia katika mkataba na:

Google LLC
imepangwa kwa mujibu wa sheria za Jimbo la Delaware, Marekani na inafanya kazi kwa mujibu wa sheria za Marekani

1600 Amphitheatre Parkway
Mountain View, California 94043
Marekani

Masharti ya umri

Iwapo hujafikisha umri unaoruhusiwa kusimamia Akaunti yako mwenyewe ya Google, ni lazima uwe na ruhusa ya mzazi au mlezi anayejulikana kisheria, ya kutumia Akaunti ya Google. Tafadhali mwombe mzazi au mlezi wako anayejulikana kisheria asome sheria na masharti haya pamoja nawe.

Iwapo wewe ni mzazi au mlezi unayejulikana kisheria na unamruhusu mtoto wako atumie huduma, basi sheria na masharti haya yanatumika kwako na unawajibikia shughuli za mtoto wako kwenye huduma.

Baadhi ya huduma za Google zina masharti ya ziada ya umri jinsi inavyobainishwa katika sera na sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi.

Uhusiano wako na Google

Sheria na masharti haya yanasaidia kufafanua uhusiano kati yako na Google. Tunapozungumza kuhusu “Google,” “sisi,” “tu-,” na “yetu,” tunamaanisha Google LLC na washirika wake. Kwa jumla, tunakupa ruhusa ya kufikia na kutumia huduma zetu iwapo utakubali kufuata sheria na masharti haya, ambayo yanaonyesha jinsi biashara ya Google hufanya kazi na jinsi tunavyochuma pesa.

Mambo unayoweza kutarajia kutoka kwetu

Kutoa aina nyingi ya bidhaa zinazofaa

Tunatoa aina nyingi za huduma ambazo zinasimamiwa na sheria na masharti haya, ikiwa ni pamoja na:
  • tovuti na programu (kama vile huduma za Tafuta na Ramani)
  • mifumo (kama vile Google Shopping)
  • huduma zilizojumuishwa (kama vile Ramani zilizopachikwa kwenye tovuti au programu za kampuni nyingine)
  • vifaa (kama vile Google Nest na Pixel)

Nyingi ya huduma hizi pia zinajumuisha maudhui ambayo unaweza kuyatiririsha au kuyashughulikia.

Huduma zingine zimebuniwa ili zifanye kazi pamoja, hatua inayokurahisishia hali ya kutoka kwenye shughuli moja hadi nyingine. Kwa mfano, iwapo tukio lako la Kalenda linajumuisha anwani, unaweza kubofya anwani hiyo na programu ya Ramani inaweza kukuonyesha jinsi ya kufika huko.

Kusanidi, kuboresha na kusasisha huduma za Google

Tunaendelea kubuni vipengele na teknolojia mpya ili kuboresha huduma zetu. Kwa mfano, tunatumia akiliunde na mfumo wa mashine kujifunza ili kukupa tafsiri za moja kwa moja pamoja na kutambua na kuzuia taka na programu hasidi kwa njia bora. Kama sehemu ya juhudi hizi za kuendelea kuboresha huduma zetu, wakati mwingine tunaongeza au kuondoa vipengele na utendaji, kuongeza au kupunguza vikomo vya huduma zetu na kuanza kutoa huduma mpya au kusimamisha za zamani. Wakati huduma inahitaji au ina programu inayoweza kupakuliwa au kupakiwa mapema, programu hiyo hujisasisha kiotomatiki wakati mwingine kwenye kifaa chako pindi kipengele au toleo jipya linapopatikana. Baadhi ya huduma hukuruhusu urekebishe mipangilio yako ya masasisho ya kiotomatiki.

Iwapo tutafanya mabadiliko muhimu ambayo yataathiri vibaya utumiaji wako wa huduma zetu au iwapo tutaacha kutoa huduma fulani, tutakupa arifa adilifu ya mapema, isipokuwa katika hali za dharura kama vile kuzuia matumizi mabaya, kushughulikia mahitaji ya kisheria au kushughulikia masuala ya kiusalama na utendakazi. Pia tutakupa fursa ya kuhamisha maudhui yako kutoka kwenye Akaunti yako ya Google kupitia Google Takeout, kwa mujibu wa sheria na sera zinazotumika.

Mambo tunayotarajia kutoka kwako

Fuata sheria na masharti haya na sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi

Ruhusa tunayokupa ya kufikia na kutumia huduma zetu itaendelea kutumika mradi unatii:

Pia unakubali kwamba Sera yetu ya Faragha inatumika katika utumiaji wako wa huduma zetu. Pia tunatoa nyenzo kama vile Kituo cha Usaidizi cha Hakimiliki, Kituo cha Usalama, Kituo cha Uwazi, na ufafanuzi wa teknolojia zetu kutoka kwenye tovuti yetu ya sera ili kujibu maswali ya kawaida na kuweka matarajio kuhusu utumiaji wa huduma zetu. Hatimaye, tunaweza kutoa tahadhari na maagizo mahususi ndani ya huduma zetu – kama vile vidirisha vya mazungumzo vinavyokuarifu kuhusu taarifa muhimu.

Ingawa tunakupa ruhusa ya kutumia huduma zetu, tunahifadhi haki zozote za uvumbuzi tulizonazo kwenye huduma.

Kuheshimu watu wengine

Tungependa kudumisha mazingira yenye heshima kwa kila mtu, hali inayomaanisha kuwa lazima ufuate kanuni hizi za msingi za matendo:
  • kutii sheria zinazotumika, ikiwa ni pamoja sheria za udhibiti wa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi, vikwazo na ulanguzi wa watu
  • kuheshimu haki za wengine, ikiwa ni pamoja na faragha na haki za uvumbuzi
  • usidhulumu au kudhuru wengine au kujidhuru (au kutishia au kuhimiza dhuluma au madhara kama hayo) — kwa mfano, kwa kupotosha, kulaghai, kuiga kinyume na sheria, kuweka kashfa, kuchokoza, kunyanyasa au kuwanyatia wengine

Sheria na masharti na sera zetu za ziada za huduma mahususi, kama vile Sera yetu Dhidi ya Matumizi Yasiyoruhusiwa ya AI Zalishi, zinatoa maelezo ya ziada kuhusu mwenendo unaofaa ambao kila mtu anayetumia huduma hizo lazima aufuate. Ikiwa utabaini kuwa watu wengine hawafuati amri hizi, huduma zetu nyingi zinakuruhusu uripoti matumizi mabaya. Ikiwa tutachukua hatua kutokana na ripoti ya matumizi mabaya, tutatoa pia mchakato wa hatua hiyo jinsi inavyoelezwa katika sehemu ya Kuchukua hatua iwapo kuna matatizo.

Usitumie vibaya huduma zetu

Watu wengi wanaofikia au kutumia huduma zetu wanaelewa kanuni za jumla zinazofanya intaneti iwe salama na wazi. Lakini inasikitisha kuwa, baadhi ya watu hawaheshimu kanuni hizo, kwa hivyo tunazieleza hapa ili tulinde watumiaji na huduma zetu dhidi ya kutumiwa vibaya. Kwa nia hiyo:

Hupaswi kutumia vibaya, kuharibu, kukatiza, au kuingilia huduma au mifumo yetu — kwa mfano, kwa:
  • kuweka programu hasidi
  • kutuma taka, kudukua au kukwepa mifumo au hatua zetu za ulinzi
  • kubadilisha mfumo ili kuondoa vizuizi vilivyowekwa na mtengenezaji, kutuma kidokezo hasidi, au kupachika kidokezo, isipokuwa kama sehemu ya mipango yetu ya usalama na majaribio ya hitilafu
  • kufikia au kutumia huduma au maudhui yetu kwa njia za ulaghai au udanganyifu, kama vile:
    • wizi wa data binafsi
    • kutayarisha maudhui au kufungua akaunti bandia, ikiwa ni pamoja na maoni bandia
    • kuwapotosha wengine ili wafikirie kuwa maudhui yaliyotokana na AI zalishi yalitayarishwa na binadamu
    • kutoa huduma zinazoonekana kuwa ni zako (au za mtu mwingine) ilhali ukweli ni kuwa zimetoka kwetu
  • kutoa huduma zinazoonekana kuwa zimetoka kwetu ilhali sivyo
  • kutumia huduma zetu (ikiwa ni pamoja na maudhui ambayo huduma hizo hutoa) kukiuka haki za kisheria za mtu, kama vile mali ya uvumbuzi au haki za faragha
  • kufanya utafiti wa kihandisi kwenye huduma au teknolojia yetu kuu, kama vile mifumo yetu ya mashine kujifunza, ili kupata siri za kibiashara au maelezo mengine tunayomiliki, isipokuwa kama inavyoruhusiwa na sheria inayotumika
  • kutumia njia za kiotomatiki kufikia maudhui kutoka kwenye huduma zetu zozote kwa kukiuka maagizo yanayoweza kusomwa kwa mashine yaliyo kwenye kurasa zetu za wavuti (kwa mfano faili za robots.txt zisizoruhusu kutambaa, mafunzo au shughuli nyingine)
  • kutumia maudhui ambayo yametayarishwa kwa AI kutoka kwenye huduma zetu kutengeneza mifumo ya mashine kujifunza au teknolojia zinazohusiana za AI
  • kuficha au kuwakilisha kwa uongo utambulisho wako ili kukiuka masharti haya
  • kutoa huduma zinazowahimiza wengine kukiuka masharti haya

Ruhusa ya kutumia maudhui yako

Baadhi ya huduma zetu zinakuruhusu upakie, uwasilishe, uhifadhi, utume, upokee au ushiriki maudhui yako. Huna wajibu wowote wa kuweka maudhui yoyote kwenye huduma zetu na una uhuru wa kuchagua maudhui ambayo ungependa kuweka. Iwapo utaamua kupakia au kushiriki maudhui, tafadhali hakikisha kuwa una haki zinazohitajika kufanya hivyo na kuwa maudhui ni halali.

Leseni

Maudhui yako husalia kuwa yako, yaani unahifadhi haki zozote za uvumbuzi ulizonazo kwenye maudhui. Kwa mfano, una haki za uvumbuzi katika maudhui bunifu unayotengeneza, kama vile maoni unayotoa. Au, unaweza kuwa na haki ya kushiriki maudhui bunifu ya mtu mwingine iwapo amekupa ruhusa.

Tunahitaji ruhusa yako iwapo haki zako za uvumbuzi zinatuzuia kutumia maudhui yako. Unaipa Google ruhusa hiyo kupitia leseni hii.

Mambo yanayoshughulikiwa

Leseni hii inashughulikia maudhui yako iwapo maudhui hayo yanalindwa kwa haki za uvumbuzi.

Mambo ambayo hayashughulikiwi

  • Leseni hii haiathiri haki zako za faragha — inahusu tu haki zako za uvumbuzi
  • Leseni hii haishughulikii aina hizi za maudhui:
    • maelezo ya kweli yanayopatikana kwa umma ambayo unatoa, kama vile masahihisho kwenye anwani ya biashara za karibu. Maelezo hayo hayahitaji leseni kwa sababu yanazingatiwa kuwa maarifa ya kawaida ambayo kila mtu ana uhuru wa kuyatumia.
    • maoni unayotoa, kama vile mapendekezo ya kuboresha huduma zetu. Maoni yanashughulikiwa katika sehemu ya Mawasiliano yanayohusiana na huduma hapa chini.

Upeo

Leseni hii:
  • inatumika ulimwenguni kote, yaani inakubaliwa mahali popote ulimwenguni
  • si ya kipekee, yaani unaweza kutoa leseni ya maudhui yako kwa watu wengine
  • haina mrabaha, yaani hamna ada kwa leseni hii

Haki

Leseni hii inairuhusu Google:

  • kupangisha, kutengeneza upya, kusambaza, kuwasiliana na kutumia maudhui yako — kwa mfano, kuhifadhi maudhui yako kwenye mifumo yetu na kufanya yapatikane popote uendapo
  • kuchapisha, kutumia au kuonyesha maudhui yako hadharani, iwapo umeyafanya yaonekane kwa watu wengine
  • kubadilisha na kubuni miigo ya kazi zinazotokana na maudhui yako, kama vile kubadilisha muundo au kuyatafsiri
  • kutoa haki hizi za kijileseni kwa:
    • watumiaji wengine waruhusu huduma ifanye kazi jinsi inavyopaswa, kama vile kukuruhusu ushiriki picha na watu unaowachagua
    • makontrakta wetu ambao wameweka sahihi makubaliano nasi ambayo yanafuata sheria na masharti haya, kwa madhumuni machache yanayobainishwa tu katika sehemu ya Madhumuni hapa chini

Madhumuni

Leseni hii inatumika kwa madhumuni machache ya:

  • kuendesha na kuboresha huduma, yaani kuruhusu huduma kufanya kazi jinsi inavyopaswa na kutengeneza vipengele na utendaji mpya. Hii ni pamoja na kutumia algoriti na mifumo otomati ili kuchanganua maudhui yako:
    • kwa taka, programu hasidi na maudhui haramu
    • kutambua mitindo katika data, kama vile kubaini wakati wa kupendekeza albamu mpya katika programu ya Picha kwenye Google ili kuweka picha zinazohusiana pamoja
    • ili kufanya huduma zetu zikufae zaidi, kama vile kukupa mapendekezo, matangazo, maudhui na matokeo ya utafutaji yanayokufaa zaidi, (ambayo unaweza kubadilisha au kuzima katika Mipangilio ya Matangazo)
    Uchambuzi huu hutokea wakati maudhui yanatumwa, kupokewa, na wakati yanahifadhiwa.
  • kutumia maudhui ambayo umeshiriki hadharani ili kutangaza huduma. Kwa mfano, ili kutangaza programu ya Google, tunaweza kunukuu maoni uliyotoa. Au, ili kutangaza Google Play, tunaweza kuonyesha picha ya skrini ya programu uliyoweka katika Duka la Google Play.
  • kubuni teknolojia na huduma mpya za Google kwa kuzingatia sheria na masharti haya

Muda

Leseni hii inatumika kwa kipindi chote ambapo maudhui yako yanalindwa kwa haki za uvumbuzi.

Iwapo utaondoa maudhui yoyote yanayoshughulikiwa na leseni hii kwenye huduma zetu, basi mifumo yetu itaondoa maudhui hayo hadharani kwa muda adilifu. Kuna hali mbili zisizofuata kanuni:

  • Iwapo tayari ulishiriki maudhui yako na watu wengine kabla ya kuyaondoa. Kwa mfano, iwapo ulishiriki picha na rafiki ambaye baadaye alitoa nakala yake au kuishiriki tena, basi picha hiyo inaweza kuendelea kuonekana kwenye Akaunti ya Google ya rafiki yako hata baada ya kuiondoa kwenye Akaunti yako ya Google.
  • Ukifanya maudhui yako yapatikane kupitia huduma za kampuni zingine, kuna uwezekano kuwa mitambo ya kutafuta, ikiwa ni pamoja na huduma ya Tafuta na Google, itaendelea kupata na kuonyesha maudhui yako kama sehemu ya matokeo yake ya utafutaji.

Kutumia huduma za Google

Akaunti yako ya Google

Iwapo unatimiza masharti haya ya umri unaweza kufungua Akaunti ya Google unapohitaji. Baadhi ya huduma zinahitaji uwe na Akaunti ya Google ili ziweze kufanya kazi — kwa mfano, ili utumie Gmail, unahitaji Akaunti ya Google ili uwe na mahali pa kutuma na kupokea barua pepe yako.

Unawajibikia shughuli unazofanya kwenye Akaunti yako ya Google, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua zinazofaa za kulinda usalama wa Akaunti yako ya Google. Tunakuhimiza utumie tovuti ya Ukaguzi wa Usalama mara kwa mara.

Kutumia huduma za Google kwa niaba ya shirika au biashara

Mashirika mengi, kama vile biashara, mashirika yasiyo ya faida na shule, hupata manufaa ya huduma zetu. Ili utumie huduma zetu kwa niaba ya shirika:
  • ni lazima mwakilishi aliyeidhinishwa wa shirika hilo akubali sheria na masharti haya
  • msimamizi wa shirika lako anaweza kukukabidhi Akaunti ya Google. Msimamizi huyo anaweza kutaka ufuate kanuni za ziada na anaweza kufikia au kufunga Akaunti yako ya Google.

Mawasiliano yanayohusiana na huduma

Ili kukupa huduma zetu, wakati mwingine huwa tunakutumia matangazo ya huduma na maelezo mengine. Ili upate maelezo zaidi kuhusu jinsi tunavyowasiliana nawe, angalia Sera ya Faragha ya Google.

Iwapo utachagua kutupa maoni, kama vile mapendekezo ya kuboresha huduma zetu, tunaweza kuchukua hatua kutokana na maoni yako bila kuwa na wajibu wowote kwako.

Maudhui katika huduma za Google

Maudhui yako

Baadhi ya huduma zetu zinakuruhusu uzalishe maudhui asili. Google haitadai umiliki wa maudhui hayo.

Baadhi ya huduma zetu hukupa fursa ya kufanya maudhui yako yapatikane kwa umma — kwa mfano, unaweza kuchapisha bidhaa au maoni ya mkahawa uliyoandika au unaweza kupakia chapisho kwenye blogu ambalo umetunga.

  • Angalia sehemu ya Ruhusa ya kutumia maudhui yako ili upate maelezo zaidi kuhusu haki zako katika maudhui yako na jinsi maudhui yako yanavyotumika kwenye huduma zetu
  • Angalia sehemu ya Kuondoa maudhui yako ili upate maelezo ya sababu na jinsi tunavyoweza kuondoa maudhui yaliyotengenezwa na watumiaji kwenye huduma zetu

Iwapo unafikiri kuwa mtu fulani anakiuka haki zako za uvumbuzi, unaweza kutuma ilani ya ukiukaji na tutachukua hatua zinazofaa. Kwa mfano, huwa tunasimamisha au kufunga Akaunti ya Google ya watu wanaokiuka hakimiliki mara kwa mara jinsi inavyobainishwa katika Kituo chetu cha Usaidizi wa Hakimiliki.

Maudhui ya Google

Baadhi ya huduma zetu ni pamoja na maudhui yanayomilikiwa na Google — kwa mfano, michoro mingi unayoona kwenye Ramani za Google. Unaweza kutumia maudhui ya Google jinsi inavyoruhusiwa na sheria na masharti haya na sheria na masharti yoyote ya ziada ya huduma mahususi, lakini tunahifadhi haki zozote za uvumbuzi tulizonazo katika maudhui yetu. Usiondoe, kuficha au kubadilisha chapa, nembo au ilani zetu zozote za kisheria. Iwapo ungependa kutumia nembo au chapa zetu, tafadhali angalia ukurasa wa Ruhusa za Chapa za Google.

Maudhui mengine

Mwisho, baadhi ya huduma zetu zinakupa uwezo wa kufikia maudhui ya watu au mashirika mengine — kwa mfano, maelezo ya mmiliki wa duka kuhusu biashara yake mwenyewe au makala ya gazeti yanayoonyeshwa kwenye Google News. Hupaswi kutumia maudhui haya bila ruhusa ya mtu au shirika hilo au bila ruhusa ya kisheria. Maoni yanayotolewa kwenye maudhui ya watu au mashirika mengine ni yao na huenda hayawakilishi maoni ya Google.

Programu katika huduma za Google

Baadhi ya huduma zetu ni pamoja na programu zinazoweza kupakuliwa au zinazopakiwa mapema. Tunakupa ruhusa ya kutumia programu hiyo kama sehemu ya huduma.

Leseni tunayokupa:
  • inatumika ulimwenguni kote, yaani inakubaliwa mahali popote ulimwenguni
  • si ya kipekee, kumaanisha tunaweza kuruhusu utumiaji wa programu hii kwa wengine
  • haina mrabaha, yaani hamna ada kwa leseni hii
  • ni ya binafsi, yaani haiwezi kutumiwa na mtu mwingine
  • haiwezi kukabidhiwa mtu mwingine, yaani huruhusiwi kumkabidhi mtu mwingine leseni hii

Baadhi ya huduma zetu ni pamoja na programu ambayo inatolewa chini ya sheria na masharti ya leseni ya programu huria ambayo tunakupa. Wakati mwingine kuna sheria katika leseni ya programu huria ambayo inabatilisha kwa njia ya wazi sehemu za sheria na masharti haya, kwa hivyo tafadhali hakikisha kuwa unasoma leseni hizo.

Hupaswi kunakili, kubadilisha, kusambaza, kuuza au kupangisha sehemu yoyote ya huduma au programu zetu.

Iwapo kutatokea tatizo au kutokubaliana

Kanusho la dhima

Tulijijengea sifa nzuri kwa kutoa huduma muhimu na za kutegemewa kama vile huduma za Tafuta na Ramani za Google, na tunaendelea kuboresha huduma zetu ili kutimiza mahitaji yako. Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria, tunatoa huduma bila dhima isipokuwa ibainishwe dhahiri katika sheria na masharti yetu ya ziada ya huduma mahususi. Sheria inatutaka tufafanue hili kwa kutumia lugha mahususi ya kisheria na tutumie herufi kubwa ili kusaidia kuhakikisha kuwa unaiona, ifuatavyo:

KWA MUJIBU WA SHERIA ZINAZOTUMIKA, TUNATOA HUDUMA ZETU “JINSI ZILIVYO” BILA ARABUNI ZOZOTE ZA MOJA KWA MOJA AU ZISIZOTAJWA, IKIWA NI PAMOJA NA ARABUNI ZISIZOTAJWA ZA UBORA KWA MAUZO, KUFAA KATIKA MADHUMUNI FULANI NA BILA UKIUKAJI. KWA MFANO, HATUBUNI DHIMA ZOZOTE KUHUSU MAUDHUI AU VIPENGELE VYA HUDUMA, IKIWA NI PAMOJA NA USAHIHI, UWEZO WA KUTEGEMEWA, UPATIKANAJI AU UWEZO WA KUTIMIZA MAHITAJI YAKO.

USITEGEMEE HUDUMA KWA USHAURI WA KIMATIBABU, KISHERIA, KIFEDHA AU USHAURI MWINGINE WA KITAALAMU. MAUDHUI YOYOTE KUHUSU MADA HIZO YAMETOLEWA KWA MADHUMUNI YA MAELEZO PEKEE NA HAYAPASWI KUTUMIKA BADALA YA USHAURI WA MTAALAMU ALIYEHITIMU.

Dhima

Kwa watumiaji wote

Sheria pamoja na sheria na masharti haya hujaribu kuleta usawa kati ya kile ambacho wewe au Google mnaweza kudaiana kukiwa na matatizo. Ndiyo maana sheria inamtaka kila mtu kuwajibikia wajibu fulani — lakini si mwingine — chini ya masharti haya.

Sheria na masharti haya yanadhibiti tu wajibu wetu kwa mujibu wa sheria inayotumika. Masharti haya hayadhibiti dhima ya kiasi cha juu cha ulegevu au matendo yasiyofaa yanayofanywa kimakusudi.

Kwa mujibu wa sheria inayotumika:
  • Google inawajibikia tu ukiukaji wake wa sheria na masharti haya au sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi
  • Google haiwajibikii:
    • kupoteza faida, mapato, fursa za biashara, sifa au akiba inayokisiwa
    • hasara za kuambatana
    • fidia za adhabu
  • Jumla ya dhima ya Google inayotokana au inayohusiana na sheria na masharti haya inapaswa kuwa zaidi ya, (1) $200 au (2) ada inayolipwa ili kutumia huduma zinazofaa kwa miezi 12 kabla ya mzozo

Kwa watumiaji wa kibiashara na mashirika pekee

Iwapo wewe ni mtumiaji wa kibiashara au shirika:

  • Kwa mujibu wa sheria inayotumika, utafidia Google na wasimamizi, maafisa, wafanyakazi na wakandarasi wake kwa kesi yoyote ya kisheria ya washirika wengine (ikiwa ni pamoja na vitendo vya mamlaka za serikali) inayotokana au inayohusiana na utumiaji wako wa huduma kinyume cha sheria au ukiukaji wa sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi. Fidia hii inashughulikia dhima yoyote au matumizi yanayotokana na madai, hasara, uharibifu, maamuzi ya korti, faini, gharama za manza na ada za kisheria.
  • Iwapo umeruhusiwa kisheria usitende majukumu fulani, ikiwa ni pamoja na ahadi ya kulipa, basi majukumu hayo hayatumiki kwako chini ya sheria na masharti haya. Kwa mfano, Umoja wa Mataifa hupata kinga fulani za wajibu wa kisheria na sheria na masharti haya hayabatilishi kinga hizo.

Kuchukua hatua iwapo matatizo yatatokea

Kabla ya kuchukua hatua kama ilivyoelezwa hapa chini, tutakupa arifa ya mapema panapowezekana kwa njia adilifu, tukueleze sababu iliyofanya tuchukue hatua na tukupe fursa ya kufafanua tatizo na kulirekebisha, isipokuwa ikiwa kufanya hivyo kunaweza:

  • kusababisha madhara au dhima kwa mtumiaji, mtu au kampuni nyingine au Google
  • kukiuka sheria au amri ya mamlaka ya utekelezaji wa sheria
  • kuathiri uchunguzi
  • kuathiri uendeshaji, maadili au usalama wa huduma zetu

Kuondoa maudhui yako

Iwapo maudhui yako yoyote (1) yanakiuka sheria na masharti haya, sera au sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi, (2) yanakiuka sheria inayotumika au (3) yanaweza kuwadhuru watumiaji wetu, washirika wengine au Google, basi tunahifadhi haki ya kuondoa baadhi ya maudhui au maudhui hayo yote kwa mujibu wa sheria inayotumika. Mifano ni pamoja na ponografia inayohusisha watoto, maudhui yanayofanikisha unyanyasaji au ulanguzi wa watu, maudhui ya kigaidi na maudhui yanayokiuka haki za uvumbuzi za mtu mwingine.

Kufunga au kusimamisha uwezo wako wa kufikia huduma za Google

Bila kuwekea kikomo haki zetu zozote zingine, Google inaweza kusimamisha au kufunga ufikiaji wako wa huduma au kufuta Akaunti yako ya Google ikiwa jambo lolote kati ya yafuatayo litafanyika:

  • unapokiuka mara kwa mara au kwa kiasi kikubwa sheria na masharti, sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi
  • tunatakiwa kufanya hivyo ili kutii mahitaji ya kisheria au amri ya mahakama
  • matendo yako yanasababisha madhara au dhima kwa mtumiaji, mshirika mwingine au Google — kwa mfano, kwa kudukua, kuiba data binafsi, kunyanyasa, kutuma taka, kupotosha wengine au kukusanya maudhui ya wengine

Ili upate maelezo zaidi kuhusu kwa nini tunafunga akaunti na kinachotokea baada ya kufunga, angalia Ukurasa huu wa Kituo cha Usaidizi. Iwapo unaamini kuwa Akaunti yako ya Google imesimamishwa au kufungwa kimakosa, unaweza kukata rufaa.

Bila shaka, una uhuru wa kuacha kutumia huduma zetu wakati wowote. Iwapo utaacha kutumia huduma fulani, tutashukuru iwapo utatujulisha sababu ili tuweze kuendelea kuboresha huduma zetu.

Kusuluhisha mizozo, sheria ya serikali na mahakama

Kwa maelezo kuhusu jinsi ya kuwasiliana na Google, tafadhali tembelea ukurasa wetu wa mawasiliano.

Sheria ya California itasimamia mizozo yote inayotokana au inayohusiana na sheria na masharti haya, sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi au huduma zozote zinazohusiana, bila kujali ukinzani wa kanuni za sheria. Mizozo hii itasuluhishwa kwa njia ya kipekee katika mahakama za nchi au jimbo la Santa Clara, California, Marekani na wewe na Google mnakubali uamuzi wa eneo la mamlaka katika mahakama hizo.

Kuhusu sheria na masharti haya

Kwa mujibu wa sheria, una haki fulani ambazo haziwezi kudhibitiwa na mkataba kama vile sheria na masharti haya. Sheria na masharti haya hayanuii kwa njia yoyote kudhibiti haki hizo.

Sheria na masharti haya yanafafanua uhusiano kati yako na Google. Hayabuni haki zozote za kisheria kwa watu au mashirika mengine, hata kama wengine wananufaika kutokana na uhusiano huo chini ya sheria na masharti haya.

Tunataka kufanya sheria na masharti haya yawe rahisi kueleweka, kwa hivyo tumetumia mifano kutoka kwenye huduma zetu. Lakini huenda si bidhaa zote zilizotajwa zinapatikana katika nchi uliko.

Iwapo sheria na masharti haya yanakinzani na sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi, sheria na masharti ya ziada yatatumika kwa huduma hiyo.

Ikitokea kwamba sheria na masharti fulani hayatumiki au hayawezi kutekelezwa, hali hii haitaathiri sheria na masharti mengine yoyote.

Iwapo hufuati sheria na masharti haya au sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi na hatuchukui hatua moja kwa moja, hiyo haimaanishi kuwa tunaachilia haki ambazo huenda tunazo, kama vile kuchukua hatua baadaye.

Tunaweza kusasisha sheria na masharti haya na sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi (1) ili kulingana na mabadiliko kwenye huduma zetu au jinsi tunavyofanya biashara — kwa mfano, tunapoweka huduma, vipengele, teknolojia, bei au manufaa mapya (au kuondoa za zamani), (2) kwa sababu za usalama, udhibiti au sheria (3) ili kuzuia madhara au matumizi mabaya.

Iwapo tutafanya mabadiliko muhimu kwenye sheria na masharti haya au sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi, tutakupa arifa adilifu ya mapema na fursa ya kukagua mabadiliko, isipokuwa (1) tunapozindua huduma au kipengele kipya au (2) katika hali za dharura, kama vile kuzuia matumizi mabaya yanayoendelea au kutimiza mahitaji ya kisheria. Iwapo hukubali sheria na masharti mapya, unapaswa kuondoa maudhui yako na uache kutumia huduma hizi. Unaweza pia kutamatisha uhusiano wako nasi wakati wowote kwa kufunga Akaunti yako ya Google. Iwapo utafunga Akaunti yako ya Google kisha ufikie au utumie huduma zetu bila akaunti, utakuwa ukifikia na kutumia huduma hizo kwa mujibu wa toleo jipya zaidi la masharti haya.

Ufafanuzi

chapa ya biashara

Ishara, majina na picha zinazotumika katika biashara ambazo zinaweza kutofautisha bidhaa au huduma za shirika au mtu binafsi au shirika na zile za mtu au shirika lingine.

dhamana

Hakikisho kuwa bidhaa au huduma itakuwa na utendaji wa kiwango fulani.

dhima

Hasara zinazotokana na aina yoyote ya madai ya kisheria, iwe madai yanatokana na mkataba, sheria za ulegevu (ikiwa ni pamoja na ulegevu) au sababu zingine na iwapo hasara hizo zingeweza au hazingeweza kutarajiwa au kutabiriwa kwa njia adilifu.

fidia

Wajibu wa kimkataba wa shirika au mtu binafsi wa kufidia hasara zinazopatikana kwa shirika au mtu binafsi kutokana na utaratibu wa mahakama kama vile kesi.

haki za uvumbuzi (hataza)

Haki za kazi za akili ya mtu, kama vile ubunifu (haki za hataza); kazi za fasihi na sanaa (hakimiliki); usanifu (haki za usanifu); na ishara, majina na picha zinazotumika katika biashara (chapa za biashara). Haki za uvumbuzi zinaweza kumilikiwa na wewe, mtu mwingine au shirika.

Haki ya kisheria ambayo inamruhusu mtayarishi wa kazi halisi (kama vile picha, video chapisho kwenye blogu) kuamua iwapo na jinsi kazi hiyo halisi inaweza kutumiwa na watu wengine, kwa mujibu wa masharti na hali fulani zisizofuata kanuni (kama vile "matumizi ya haki" na "matumizi yasiyo ya biashara").

huduma

Huduma za Google zinazotegemea sheria na masharti haya ni huduma na bidhaa zilizoorodheshwa katika https://policies.google.com/terms/service-specific, ikiwa ni pamoja na:

  • tovuti na programu (kama vile Tafuta na Ramani)
  • mifumo (kama vile Google Shopping)
  • huduma zilizojumuishwa (kama vile Ramani zilizopachikwa kwenye programu au tovuti za kampuni zingine)
  • vifaa na bidhaa nyingine (kama vile Google Nest)

Nyingi ya huduma hizi pia zinajumuisha maudhui ambayo unaweza kuyatiririsha au kuyashughulikia.

kanusho

Taarifa inayodhibiti majukumu ya kisheria ya mtu.

maudhui yako

Mambo unayobuni, kupakia, kuwasilisha, kuhifadhi, kutuma, kupokea au kushiriki ukitumia huduma zetu kama vile:

  • Hati, Majedwali ya Google na Slaidi za Google unazotengeneza
  • machapisho kwenye blogu unayopakia kupitia Blogger
  • maoni unayotoa kupitia Ramani
  • video unazohifadhi kwenye Hifadhi
  • barua pepe unazotuma na kupokea kupitia Gmail
  • picha unazoshiriki na marafiki kupitia programu ya Picha
  • ratiba za usafiri unazoshiriki na Google

mshirika

Shirika ambalo liko kwenye kikundi cha kampuni za Google, yaani Google LLC na kampuni inazomiliki, ikiwa ni pamoja na kampuni zifuatazo ambazo zinatoa huduma kwa watumiaji katika Umoja wa Ulaya: Google Ireland Limited, Google Commerce Limited na Google Dialer Inc.

mtumiaji

Mtu binafsi anayetumia huduma za Google kwa madhumuni ya kibinafsi na yasiyo ya kibiashara nje ya soko, biashara, fani au taaluma yake. (Angalia mtumiaji wa kibiashara)

mtumiaji wa kibiashara

Shirika au mtu binafsi ambaye si mtumiaji (angalia watumiaji).

shirika

Shirika la kisheria (kama vile kampuni, shirika lisilo la faida au shule) wala si mtu binafsi.

toleo la nchi

Iwapo una Akaunti ya Google, tunahusisha akaunti yako na nchi (au eneo) ili tuweze kubaini:

  • mshirika wa Google anayekupa huduma na anayechakata taarifa zako unapotumia huduma
  • toleo la sheria na masharti yanayoongoza uhusiano wetu

Ukiwa umeondoka kwenye akaunti, toleo la nchi uliko hubainishwa na mahali ambako unatumia Huduma za Google. Iwapo una akaunti, unaweza kuingia na usome sheria na masharti haya ili uone nchi inayohusishwa nayo.

Programu za Google
Menyu kuu