Jinsi Google inavyotumia vidakuzi

Kidakuzi ni aina ndogo ya maandishi yanayotumwa kwenye kivinjari chako na tovuti unayotembelea. Husaidia tovuti ikumbuke maelezo kuhusu ulikotembelea, hali inayoweza kurahisisha mchakato wa kutembelea tovuti tena na kufanya tovuti ikufae zaidi.

Kwa mfano, tunatumia vidakuzi kukumbuka lugha unayopendelea, kufanya matangazo unayoona yakufae zaidi, kuhesabu idadi ya wageni wanaotembelea ukurasa, kukusaidia kujisajili kwenye huduma zetu, kulinda data yako na kukumbuka mipangilio yako ya matangazo.

Ukurasa huu unafafanua aina za vidakuzi vinavyotumiwa na Google. Unaelezea pia jinsi Google na washirika wetu hutumia vidakuzi katika utangazaji. Angalia Sera ya Faragha ili upate maelezo kuhusu jinsi tunavyolinda faragha yako katika matumizi yetu ya vidakuzi na maelezo mengine.

Aina ya vidakuzi vinavyotumiwa na Google

Baadhi ya vidakuzi au vidakuzi vyote vilivyofafanuliwa hapa chini vinaweza kuhifadhiwa kwenye kivinjari chako. Ili udhibiti jinsi vidakuzi vinatumiwa, unaweza kukataa kutumia vidakuzi fulani kupitia mipangilio yako ya kuweka mapendeleo kwenye Google wakati wowote kwa kutembelea g.co/privacytools. Unaweza pia kudhibiti vidakuzi kwenye kivinjari chako (ingawa huenda vivinjari vya vifaa vya mkononi visiwe na uonekanaji huu). Kwa mfano, ikiwa unatumia Google Chrome kama kivinjari chako, unaweza kutembelea chrome://settings/cookies.

Utendaji

Vidakuzi vinavyotumiwa katika utendaji huruhusu watu watumie huduma au tovuti ili kufikia vipengele vya msingi vya huduma hiyo. Mambo yanayochukuliwa kuwa ya msingi kwenye huduma ni pamoja na mapendeleo kama vile chaguo la lugha ya mtumiaji, maboresho ya bidhaa yanayosaidia kudumisha na kuimarisha huduma na kuhifadhi maelezo yanayohusiana na kipindi cha mtumiaji, kama vile bidhaa zilizo kwenye kikapu cha ununuzi.

Baadhi ya vidakuzi hutumiwa kuhifadhi mapendeleo ya watumiaji. Kwa mfano, watu wengi wanaotumia huduma za Google wana kidakuzi kinachoitwa 'NID' katika vivinjari vyao. Kidakuzi hiki kina kitambulisho cha kipekee tunachotumia kukumbuka mapendeleo yako na maelezo mengine, kama vile lugha unayopendelea, idadi ya matokeo ya utafutaji ambayo ungependa yaonyeshwe kwenye ukurasa wa matokeo (kwa mfano, 10 au 20) na iwapo ungependa kuwasha kichujio cha Utafutaji Salama kwenye Google. Muda wa kila kidakuzi cha NID huisha baada ya miezi sita, kuanzia wakati kinatumiwa mara ya mwisho na mtumiaji. Kidakuzi kinachoitwa ‘VISITOR_INFO1_LIVE’ hufanya kazi sawa kwenye YouTube na pia hutumiwa kutambua na kutatua matatizo katika huduma.

YouTube hutumia kidakuzi cha ‘PREF’ kuhifadhi maelezo kama vile mipangilio ya ukurasa inayopendelewa na mtumiaji na mapendeleo ya uchezaji kama vile kucheza kiotomatiki, kuchanganya maudhui na ukubwa wa kichezaji. Kwenye YouTube Music, mapendeleo haya yanajumuisha kiwango cha sauti, hali ya kujirudia na kucheza kiotomatiki. Muda wa kidakuzi hiki huisha miezi minane kuanzia kinapotumiwa mara ya mwisho na mtumiaji.

Baadhi ya vidakuzi hutumiwa kudumisha na kuboresha hali ya utumiaji katika kipindi mahususi cha kuvinjari. Kwa mfano, ‘YSC’ hutumiwa na YouTube kukumbuka data ya mtumiaji na hulinganisha vitendo vya mtumiaji. Kidakuzi hiki huendelea kutumika mradi mtumiaji hajafunga kivinjari chake. Kidakuzi cha ‘pm_sess’ pia husaidia kudumisha kipindi cha mtumiaji kwenye kivinjari na hudumu kwa dakika 30.

Baadhi ya vidakuzi huboresha utendaji wa huduma za Google. Kwa mfano, ‘CGIC’ huboresha uwekaji wa matokeo ya utafutaji kwa kukamilisha kiotomatiki hoja za utafutaji kulingana na data ya awali ya mtumiaji. Kidakuzi hiki hudumu kwa miezi sita.

Usalama

Vidakuzi vinavyotumiwa kwa ajili ya usalama huthibitisha watumiaji, kuzuia ulaghai na kulinda watumiaji wanapotumia huduma.

Baadhi ya vidakuzi hutumiwa kuthibitisha watumiaji, hali inayosaidia kuhakikisha kuwa mmiliki halisi ndiye pekee anayeweza kufikia akaunti hiyo. Kwa mfano, vidakuzi vinavyoitwa ‘SID’ na ‘HSID’ huwa na rekodi zilizotiwa saini dijitali na zilizosimbwa kwa njia fiche, za kitambulisho cha Akaunti ya Google ya mtumiaji na muda wa hivi karibuni zaidi wa kuingia katika akaunti. Mseto wa vidakuzi hivi huturuhusu kuzuia aina nyingi za mashambulizi, kama vile majaribio ya kuiba maudhui ya fomu zinazotumwa kwenye huduma za Google.

Baadhi ya vidakuzi hutumiwa kuzuia taka, ulaghai na matumizi mabaya. Kwa mfano, vidakuzi vya ‘pm_sess’ na ‘YSC’ huhakikisha kuwa maombi katika kipindi cha kuvinjari yamefanywa na mtumiaji wala si na tovuti nyingine. Vidakuzi vyote viwili huzuia tovuti hasidi zisitende bila mtumiaji kujua na zisiige mtumiaji huyo.

Takwimu

Vidakuzi vinavyotumiwa kwenye takwimu husaidia kukusanya data inayoruhusu huduma zielewe jinsi watumiaji wanavyotumia huduma mahususi. Maarifa haya huruhusu huduma kuboresha maudhui na kubuni vipengele bora ambavyo huboresha hali ya utumiaji.

Baadhi ya vidakuzi husaidia tovuti kufahamu jinsi wageni wao wanavyotumia tovuti na programu. Kwa mfano, Google Analytics, bidhaa ya Google inayosaidia wamiliki wa tovuti na programu kuelewa jinsi watu wanavyotumia huduma, hutumia kundi la vidakuzi kukusanya maelezo na kuripoti takwimu za matumizi ya tovuti bila kutambulisha wageni mahususi kwenye Google. ‘_ga’ ndicho kidakuzi kikuu kinachotumiwa na Google Analytics. ‘_ga’ huwezesha huduma zitofautishe kati ya mtumiaji mmoja na mwingine na hudumu kwa miaka miwili. Hutumiwa na tovuti yoyote inayotekeleza Google Analytics, zikiwemo huduma za Google.

Huduma za Google pia hutumia vidakuzi vya takwimu kama hivi, pamoja na vingine kama vile ‘NID’ kwenye huduma ya Tafuta na Google na ‘VISITOR_INFO1_LIVE’ kwenye YouTube.

Matangazo

Google hutumia vidakuzi katika utangazaji, ikiwemo kuonyesha na kutekeleza matangazo, kuweka mapendeleo kwenye matangazo (kulingana na mipangilio yako ya matangazo katika g.co/adsettings), kudhibiti mara ambazo tangazo huonyeshwa kwa mtumiaji, kuzima matangazo ambayo umechagua kuacha kuona na kupima ufaafu wa matangazo.

  • ‘NID’ hutumiwa kwa madhumuni haya ili kuonyesha matangazo ya Google katika huduma za Google kwa watumiaji ambao wameondoka kwenye akaunti
  • ‘IDE’ na ‘ANID’ hutumiwa kwa madhumuni haya ili kuonyesha matangazo ya Google kwenye tovuti zisizo za Google

Huduma nyingine za Google kama vile YouTube zinaweza pia kutumia vidakuzi hivi na vidakuzi kama ‘VISITOR_INFO1_LIVE’ kuonyesha matangazo yanayofaa zaidi.

Iwapo umewasha mipangilio ya matangazo yanayowekewa mapendeleo, ‘ANID’ hutumiwa kukumbuka mipangilio hii na hudumu kwa miezi 13 kwenye nchi washirika katika Makubaliano ya Kiuchumi ya Ulaya (EEA), Uswizi na Uingereza (UK), na hudumu kwa miezi 24 kwingineko. Iwapo umezima mipangilio ya matangazo yanayowekewa mapendeleo, ‘ANID’ hutumiwa kuhifadhi mipangilio hiyo hadi 2030. Muda wa kidakuzi cha ‘NID’ huisha miezi sita kuanzia kinapotumiwa mara ya mwisho na mtumiaji. ‘IDE’ hudumu kwa miezi 13 kwenye nchi washirika katika Makubaliano ya Kiuchumi ya Ulaya, Uswizi na Uingereza (UK) na hudumu kwa miezi 24 kwingineko.

Baadhi ya vidakuzi ambavyo hutumiwa katika utangazaji hulenga watumiaji ambao huingia katika akaunti ili kutumia huduma za Google. Kwa mfano, ‘DSID’ hutumiwa kutambua mtumiaji ambaye ameingia katika akaunti kwenye tovuti zisizo za Google na kukumbuka iwapo mtumiaji amekubali kuweka mapendeleo ya matangazo. Hudumu kwa wiki mbili.

Kupitia mfumo wa utangazaji wa Google, biashara zinaweza kutangaza kwenye huduma za Google na pia kwenye tovuti zisizo za Google zinazoshirikiana na Google.

Baadhi ya vidakuzi huruhusu Google kuonyesha matangazo kwenye tovuti za wengine na huwekwa kwenye vikoa vya tovuti unazotembelea. Kwa mfano, ‘_gads’ huwezesha tovuti kuonyesha matangazo ya Google, ikiwa ni pamoja na matangazo yaliyowekewa mapendeleo. Vidakuzi vinavyoanza kwa ‘_gac_’ hutoka kwenye Google Analytics na hutumiwa na watangazaji kupima shughuli za watumiaji na utendaji wa kampeni zao za utangazaji. Kidakuzi cha ‘_gads’ hudumu kwa miezi 13 na vidakuzi vya ‘_gac_’ hudumu kwa siku 90.

Baadhi ya vidakuzi hutumiwa kupima utendaji wa matangazo na kampeni na asilimia ya walioshawishika kwenye matangazo ya Google katika tovuti unayotembelea. Kwa mfano, vidakuzi vinavyoanza kwa ‘_gcl_’ hutoka kwenye Google Analytics na hutumiwa kimsingi kusaidia watangazaji kubaini mara ambazo watumiaji wanaobofya matangazo yao hushawishika kuchukua hatua kwenye tovuti zao, kama vile kufanya ununuzi. Vidakuzi vinavyotumiwa kupima asilimia ya walioshawishika havitumiki kuweka mapendeleo kwenye matangazo. Vidakuzi vya ‘_gcl_’ hudumu kwa siku 90.

Kuweka Mapendeleo

Vidakuzi vinavyotumiwa kuweka mapendeleo huboresha hali ya utumiaji kwa kuweka maudhui na vipengele vinavyomfaa mtumiaji.

Kulingana na mipangilio yako katika g.co/privacytools, baadhi ya vidakuzi huwezesha mapendekezo bora kwenye huduma. Kwa mfano, ‘VISITOR_INFO1_LIVE’ huwezesha mapendekezo yaliyowekewa mapendeleo kwenye YouTube kulingana na utafutaji na utazamaji wa awali. Na ‘NID’ huwezesha vipengele vya kukamilisha kiotomatiki vilivyowekewa mapendeleo katika huduma ya Tafuta wakati watumiaji wanaandika hoja za utafutaji. Muda wa vidakuzi hivi huisha miezi sita kuanzia vinapotumiwa mara ya mwisho na mtumiaji.

Kudhibiti vidakuzi katika kivinjari chako

Vivinjari vingi hukuruhusu udhibiti jinsi vidakuzi huwekwa na kutumiwa unapovinjari na hukuruhusu kufuta data ya kuvinjari na vidakuzi. Pia, kivinjari chako kinaweza kuwa na mipangilio inayokuruhusu udhibiti vidakuzi kulingana na tovuti. Kwa mfano, mipangilio ya Google Chrome hukuruhusu ufute vidakuzi vilivyoko, uruhusu au uzuie vidakuzi vyote na uweke mapendeleo ya vidakuzi kwenye tovuti. Google Chrome pia ina Hali Fiche, ambayo haihifadhi historia yako ya Chrome ya tovuti unazotembelea au kuhifadhi vidakuzi kwenye kifaa chako baada ya kufunga Madirisha yote fiche.

Programu za Google
Menyu kuu